Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amesema hawezi kuachia
madaraka kwa sababu mazao yake yote aliyoyapanda ndiyo yanaanza kutoa matunda.
Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni za
kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini humo
, Museveni alisema akiachia madaraka kwa sasa
atakuwa hajawatendea haki raia wa Uganda.
“Wale wanaosema, ‘muache aende, muache aende’
wanapaswa kufahamu kwamba huu siyo wakati wa kufanya hivyo,” alisema Museveni
wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika wilaya ya Ntungamo
“Huyu mzee aliokoa nchi hii, mnaweza kumtaka
aondoke? Ninawezaje kuacha shamba la migomba ambayo nimeipanda mwenyewe na
limeshaanza kutoa matunda?” alihoji Museveni na kuongeza:
“Lazima tuzingatie maendeleo, wakati wangu utafika
na nitaondoka.”
Wagombea saba watashiriki kwenye kinyang’anyiro
cha urais nchini humo Februari 18 mwaka huu ili kumuondoa Museveni madarakani.
Kiongozi huyo aliyekaa madarakani tangu mwaka
1986, anachuana vikali na wapinzani wake, Dk Kizza Besigye na Amama Mbabazi,
aliyekuwa waziri mkuu.Mbabazi alisema akishinda urais atapitisha kipengele cha
muda wa rais kukaa madarakani wa vipindi viwili.
“Wakati yeye (Museveni) aliponiambia kwamba
hangestaafu na kuniomba nimuunge aendelee kuwania urais , nilisema hapana na
sasa niko hapa,” alisema Mbabazi kwenye mkutano wa kampeni nchini humo
“Katika siku100 za kwanza nikiwa rais, tutarejesha
vipindi vya rais kukaa madarakani katika katiba na tutafanya tuwezalo
kuhakikisha kuwa katika miaka mitano ya kwanza tutafanya juu chini kuandaa
kizazi chenye umri mdogo ili kitwae madaraka Uganda,” alisema Mbabazi
SOURCE Mwananchi
Post a Comment