Dalili za kufanyika kwa uchaguzi
wa Rais wa Zanzibar na wawakilishi zinaonekana kuwa finyu kutokana na
kutokuwapo maelekezo yoyote ya kuitaka Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuanza kuuandaa.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha
Salum Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo
Oktoba 28, akisema
kulikuwapo na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na kuahidi
kuwa ungeitishwa uchaguzi mpya ndani ya siku 90.
Zikiwa zimepita siku 44
tangu atangaze uamuzi huo, hakuna maelekezo yoyote kuhusu maandalizi ya
uchaguzi huo kutoka ZEC, huku kukiwa hakuna taarifa rasmi za maendeleo ya vikao
vinavyodaiwa kufanywa baina ya uongozi wa CCM na CUF, vyama vyenye upinzani
mkali visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa
ZEC, Salum Kassim Ali aliiambia Mwananchi jana kuwa hawajapata maagizo yoyote
ya kutakiwa kuanza maandalizi ya uchaguzi.
Ingawa hakuwa tayati
kuzungumzia suala hilo kwa kina, Kassim Ali alisema wakati akijibu maswali ya
gazeti hili kuwa hakuna kinachoendelea hadi sasa.
“Wewe unauliza kununua
pampasi wakati hujui mtoto atazaliwa lini? Badala ya kuuliza uchaguzi upo au
haupo unauliza vitu vingine?” alihoji Kassim Ali alipoulizwa na gazeti hili
uchaguzi wa marudio utafanyika lini”. alihoji.
Maalim Seif Sharrif Hamad
alitangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo na kuitaka ZEC imtangaze mshindi.
Kitendo hicho pamoja na vurugu ambazo Jecha alidai zilifanyika ndani ya ZEC na
wakati wa kuandikisha wapigakura, ndvyo vilivyomfanya atangaze kufuta uchaguzi,
uamuzi ambao unapingwa na CUF inayodai kuwa mwenyekiti huyo hana mamlaka ya
kufuta uchaguzi na kwamba alichukua uamuzi huo bila ya kushirikisha wajumbe
wenzake.
Kuhusu taarifa kwamba
Jecha amekuwa haonekani ofisini, mkurugenzi huyo wa uchaguzi wa ZEC alisema
taarifa hizo si za kweli na kwamba kama kuna taarifa zimeenea kuhusu jambo hilo,
ziandikwe hivyo hivyo. “Aliyekuambia hayupo ofisini ni nani? Andika hayo hayo
ya mitaani,” alisema.
Akizungumzia suala hilo
la tarehe ya uchaguzi wa marudio, ofisa uhusiano wa ZEC, Idrissa Jecha alisema
kuwa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar haizungumzii uchaguzi wa marudio bali
tarehe ya kupiga kura baada ya wagombea kuteuliwa na Tume.
SOURCE MWANANCHI
Post a Comment