0


Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyojifungia kwa siku moja, imeazimia iundwe
ngazi ya uongozi ya chama itakayojulikana kama ‘Dar es Salaam Kuu’ ili kuijenga, kuitetea na kuilinda demokrasia inayodaiwa kuelekea kuporwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema chombo hicho kimeundwa kwa mujibu wa katiba ya chama chao (Chadema).

Alisema chombo hicho ambacho kitakuwa na wajumbe 25 wakiwamo wabunge wa kuchaguliwa na wa viti maalumu, mameya, madiwani na wenyeviti; kitakuwa na kazi ya kuongeza nguvu ya usimamizi, udhibiti na uratibu wa chama.

Alisema mwenyekiti wa chombo hicho atakuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara; makamu atakuwa Diwani wa Temeke, Bernard Mwakyembe; Katibu, Henry Kileo; na mweka hazina atakuwa Susan Lyimo.

Alisema katika mchakato wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kumejengeka utamaduni wa kushtukizana bila ya kuwa na ushauriano juu ya lini uchaguzi huo unafanyika.

Madiwani wengi katika Jiji la Dar es Salaam wanatoka Chadema na Chama cha Wananchi (CUF), ambavyo hushirikiana kupitia muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). 

"Tumeona (CCM) hawana nia njema. Kwa hiyo hatutashiriki uchaguzi wa kushtukizana. Kanuni ipo wazi… inasema notisi ni siku saba ili nasi tujiandae," alisema.

Uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo kile kinachoelezwa na madiwani wa Ukawa kuwa ni mizengwe inayosababishwa na CCM inaoenekana kutokuwa tayari jiji hilo kuwa chini ya upinzani. 

Katika hatua nyingine, Mbowe ambaye pia ni Mkuu wa Kambi Ramsi ya Upinzani Bungeni, alisema katika miezi mine ya utawala wake, Serikali ya Rais John Magufuli imeyumba kwa kiasi kikubwa katika kusimamia misingi ya utawala bora. 

Alitolea mfano kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, akisema washindi halali waliochaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura hawajapewa haki yao ya kuongoza. 

“Waliochaguliwa kihalali Zanzibar hawajapewa fursa kama wananchi walivyoamua na vile vyama vinavyoshiriki uchaguzi wa marudio (utakaofanyika Machi 20) ni wakala wa CCM,” alisema.

Aidha, alisema wameshangazwa na kitendo cha kuzuiwa sehemu kubwa ya urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), ambayo ni mali ya umma.

Mbowe alisema serikali imeingilia uundwaji wa uongozi wa kamati za kusimamia fedha za umma bungeni ambazo kwa kawaida hutakiwa kuongozwa na kambi ya upinzani.

Post a Comment

 
Top