Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imezishauri Taasisi za Kibenki zilizopo nchini kuanzisha timu na vilabu vya michezo ili kukuza michezo pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana walio wengi ambao wana vipaji lakini hawana timu za kuwaendeleza.
Hayo yamebainishwa kupitia kwa Waziri mwenye dhamana, Mh. Nape Nnauye mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo tuzo za wachezaji bora walioshinda katika michezo maalum ya BRAZUKA KIBENKI iliyoandaliwa na benki ya Barclays na wadau wengine.
Waziri Nape amebainisha kuwa, Nia ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inakuza michezo na kuwa na fursa za kiuchumi kupitia michezo hivyo taasisi hizo zinazo fursa ya kuongeza ajira na ustawi mzuri wa michezo endapo zitaanzisha timu za michezo na kimashindano kwani zinaweza na zinao wajibu huo.
Kwa mujibu wa Mratibu wa michuano hiyo, Nasikiwa Berya alieleza kuwa, jumla ya timu 16 zilishiriki huku ikianza 28 Novemba 2015 na kufikia tamati 20 Februari 2016 ilikuwa ni ya aina yake na kutoa mwangaza wa kimaendeleo wa kimichezo ambapo pia imesaidia kuimarisha afya, ushikamano na undugu kwa baina ya wachezaji na washangiliaji ambao wengi wao walitoka katika mabenki shiriki 15 ikiwemo matawi yao ya Tanzania Bara na Visiwani.
Katika tukio hilo, washindi mbalimbali walipatiwa vyeti vya shukrani hii ni pamoja na wadhamini wa mashindano hayo ikiwemo kutoka mabenki, kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group) na makampuni mengine walipewa vyeti vya shukrani katika kufanikisha michuano hiyo.
Post a Comment