Baraza la Viajana wa Chadema (Bavicha) limemtaka msajili wa vyama vya siasa nchini kutoa tamko kuhusu vitendo vya ubaguzi wa rangi vilivyooneshwa na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mapinzuzi ya Zanzibar.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeye alisema kuwa kutokana na vitendo hivyo vya kibaguzi, msajili anapaswa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuifutia usajili CCM.
“Sheria ya usajili wa vyama vya siasa iko wazi. Sheria ya usajili wa vyama vya siasa inasema, chama chochote kitakachofanya siasa za kibaguzi huenda wa kikabila, kidini ama vinginevyo chama hicho kitafutwa. Tunataka kauli ya msajili wa vyama vya siasa. Ni lini, wakati gani ataifuta CCM,” alisema Simbeye.
Simbeye alisema kuwa Baraza hilo la vijana la Chadema linamtaka msajili kutoa tamko lake ndani ya kipindi cha siku tatu na kwamba asipofanya hivyo, watachukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kwenda mahakamani.
“Msajili wa vyama vya siasa atuambie ni lini sheria hiyo imeondolewa mpaka leo CCM ni chama cha siasa kwenye taifa hili. Vinginevyo, ndugu waandishi wa habari tumepanga… na haya ndio maazimio ya vuguvugu hili, tutampeleka mahakani,” alisema.
Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa CCM ulitoa tamko na kuomba radhi kwa vitendo vya kibaguzi vilivyojitokeza kwenye sherehe hizo ambavyo vilifanywa na kundi la watu wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa chama hicho. Watu hao walibeba bango lenye ujumbe wa kibaguzi.
Post a Comment