Tundu Lissu ameeleza kuwa tayari majibu ya maswali yaliyoulizwa kuhusu Edward Lowassa kuwa mali au mzigo kwenye chama hicho yamejidhihirisha wazi.
Swali hilo liliulizwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa aliyedai kuwa alishindwa kupata majibu kama ujio wa Lowassa kama anaingia kwenye chama hicho kama mzigo au mali.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita, Tundu Lissu alieleza kuwa tayari majibu hayo yako wazi kuwa Lowassa ameweza kuvipa vyama vinavyounda Ukawa uwezo wa kushika Halmashauri za jiji la Dar es Salaam hatua ambayo haijawahi kufikiwa na chama chochote cha upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Hivyo, ni mali na sio mzigo.
“Tangu upinzani uingie ncbini haujawahi kuishika Dar, Lowassa ameiteka Dar,” alisema Lissu.
Uchaguzi wa Umeya uliofanyika wikendi iliyopita uliwezesha diwani wa kata ya Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Boniface Jackob kushinda nafasi ya umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, huku nafasi ya Naibu Meya ikienda kwa Jumanne Mbulu wa Chama cha Wananchi CUF.
Kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Nafasi ya Umeya ilishikwa na Charles Kayeko wa Chadema na naibu wake ni Omari Kumbilamoto wa CUF.
Vyama vinavyounda Ukawa pia vimeweza kushika Halmashauri za majiji ya Arusha, Mbeya na Halmashauri nyingine za miji na manispaa ambazo zilikuwa mikononi mwa CCM.
Post a Comment