0


Watu wa msimbazi wameagua kilio kikubwa  sana nchini baada ya Nyumba zaidi ya 30 zimebomolewa kwa kutumia buldoza chini ya ulinzi mkali w
a askari wa Jeshi la Polisi.
Timu ya Mwanahalisionline imeshuhudia bomoabomoa hiyo na kuelezwa na wananchi kuwa serikali haithamini utu wa raia wanyonge kwa kuwa hata taarifa haikutolewa ili kupata nafasi ya kujiandaa kwa kuondoa vitu vyao.
Zulfa Yusufu amesema hawajapinga amri ya serikali isipokuwa analalamika kuwa kuwavunjia wananchi makazi yao ni kukosa ubinaadamu.
“Tumeamka asubuhi hatuna hili wala lile, mara tunaona magari ya polisi na mengineyo, ghafla wanatuambia kwa dakika 10 tuondoe vitu. Haiwezekani dakika hizo nijue wapi naenda au nini hatima yetu?”
Hassani Shabani analalamika hakupewa taarifa yoyote kuhusu operesheni hiyo na kwa hivyo amegharimika kwa kupoteza mali zake.
Mama Mkude amesema wanakabiliwa na wakati mgumu kwani hawana hata sehemu ya kwenda wala fedha ambapo wakazi wengine wamepoteza vyakula vyao, mali na kupotezana na watoto wao.
Operesheni hiyo pia ilisimamiwa na Baraza la Usimamizi na Utunzaji Mazingira (NEMC) ambalo mwanasheria wake, Machare Suguta amesema serikali ilitoa taarifa kuwa wananchi wote waliojenga mita 60 kutoka kwenye mito, mabonde na fukwe za bahari wahame kwani watu hao watakuwa ni wavamizi katika maeneo hayo.
Diwani wa Kata ya Hananasif, Ray Kimbator amesema serikali imekubali kuwafanya wananchi wao kuwa ni wakimbizi ndani ya nchi yao.
Kimbator amesema hata kama serikali ina uhalali wa kutoa amri kama hiyo, utu ungewekwa mbele kwa kuwa wananchi hawana uwezo wa kupata maeneo yanayopimwa ili wajenge nyumba za kisasa.
“Wakazi wa hapa wamekosa makazi, hawana vyakula, na pia wameingia kwenye ukimbizi ilhali wapo kwenye nchi yao,” amesema Kimbator ambaye anatokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Amesema ameongea na mwanasheria wa Halmashauri ya Kinondoni ili aweze kuwapa kibali kisheria cha kuweza kuomba kusimamishwa kwa operesheni hiyo kwa siku tatu au zaidi ili wananchi watakaoathirika wahifadhi mali zao na kuhama kwenye maeneo hayo.

Post a Comment

 
Top