Polisi mkoani Singida
inamshikilia Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste
Itaja na mkewe kwa tuhuma za
kumfungia ndani ya chumba mtoto wao mlemavu wa viungo kwa miaka 12 bila kutoka
nje.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Sin
gida, Thobias Sedoyeka aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni David Mtipa (59)
ambaye ni Mchungaji wa Kanisa hilo na mkewe Mariam Philipo (45) wote wakazi wa
kijiji cha Itaja katika tarafa ya Mgori wilayani Singida.
Kamanda Sedoyeka alisema
tukio hilo liligundulika juzi katika kijiji hicho baada ya Polisi kupata
taarifa za siri kutoka kwa wasamaria. Akielezea tukio hilo, Kamanda Sedoyeka
alisema watuhumiwa walimfungia ndani ya chumba mtoto huyo, Timotheo David (30)
kwa muda wa miaka 12 huku huduma zote za kibinadamu, ikiwemo haja ndogo na
kubwa pamoja na chakula zikifanyika humo ndani.
“Baada ya timu ya askari
wa Upelelezi na Ofisa Ustawi wa Jamii kufika eneo hilo wakiwa na viongozi wa
kijiji na kufanya mahojiano, watuhumiwa walikiri kumfungia chumbani mtoto wao
huyo na kwamba ni mlemavu wa miguu na mikono, lakini pia ni mlemavu wa akili,”
alisema Kamanda Sedoyeka na kuongeza:
“Wamesema mtoto wao
alizaliwa mwaka 1984 akiwa mzima, lakini alipofika darasa la sita 2003 alianza
kuugua ugonjwa usiojulikana ikiwa ni pamoja na kuanguka kisha kutoa povu
mdomoni huku mwili wake ukibadilika rangi kuwa ya njano na kutibiwa bila
mafanikio.”
Aidha, alisema mlemavu
huyo alitibiwa maeneo mbalimbali bila mafanikio na ndipo wazazi hao walipoamua
kumfungia ndani baada ya kuona wanafedheheshwa mbele ya jamii huku akila
chakula, kujisaidia humo chumbani na kutoruhusiwa kutoka nje.
Kutokana na hali hiyo,
majirani waliingiwa na hofu kwa kutomwona mtoto huyo kwa kipindi kirefu kiasi
hicho hali iliyozua maswali mengi. Wakati baadhi walijua huenda ameuawa,
wengine walihusisha kitendo hicho na imani za kishirikina huku Mchungaji
akidaiwa kuzidiwa maarifa na mkewe.
Alisema kitendo cha
kumfungia mtoto huyo ndani kwa kipindi chote hicho, kumwacha akiwa uchi na
kumlaza kwenye kitanda cha kamba kisichokuwa na godoro ilikuwa ni ukiukwaji wa
misingi ya binadamu na si cha kiutu.
Alisema amepelekwa
Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake
wakati wazazi hao wakishikiliwa na kuhojiwa ili hatimaye wafikishwa mahakamani
kwa ukatili uliovuka mipaka.
SOURCE HABARI LEO
Post a Comment