0
RAIS John Magufuli katika Baraza lake jipya la Mawaziri lenye idadi ya mawaziri 19, ameteua sura mpya za mawaziri 14 ambao kati yao mawaziri kamili ni wanne na manaibu waziri 10. Aidha katika baraza hilo, pia Rais aliwapandisha cheo manaibu waziri watatu na kuwa mawaziri kamili ambao katika baraza lililopita katika Serikali ya Awamu ya Nne w
alikuwa ni manaibu waziri.
Mawaziri wengine wapya ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Waziri huyo ni mara ya pili kushika wadhifa huo katika wizara hiyo, ambapo katika Serikali ya Awamu ya Nne, alijiuzulu baada ya kuibuka kwa kashfa ya fedha za akaunti ya Escrow.
Kiongozi huyo aliteuliwa ubunge na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na kukabidhiwa wadhifa huo wa Waziri wa Nishati na Madini hadi pale alipojiuzulu ambapo katika uchaguzi wa mwaka huu, aligombea ubunge kupitia Jimbo la Musoma Vijijini na kushinda.
Aidha, Dk Magufuli amemteua Balozi Dk Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa. Dk Mahiga ambaye pia katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Urais ndani ya CCM naye alikuwa ni mmoja wa watia nia na ni Mbunge wa Kuteuliwa.
Baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha Urais ndani ya CCM, kiongozi huyo aliomba kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini ambako pia alishindwa katika kura za maoni na Frederick Mwakalebela kuibuka kidedea.
Balozi Mahiga amewahi kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005).
Pamoja na Waziri huyo, pia Dk Magufuli amemteua Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi kuwa Waziri mpya wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo. Kabla ya uteuzi huo, Nape alikuwa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
Aidha Nnauye aliwahi kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Ubungo mwaka 2010 na kushindwa kwenye kura za maoni, ambapo Rais Kikwete baadaye alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi kabla ya kurejeshwa kwenye uongozi wa chama na kuwa Katibu wa Uenezi Taifa.
Aidha, manaibu waziri 10 wapya walioteuliwa katika baraza hilo ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Abdallah Possi ambaye amekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu. Dk Possi ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), anakuwa Mbunge wa Kuteuliwa.
Mwingine ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Anthony Mavunde. Mavunde ambaye ni Mbunge wa Dodoma Mjini katika wizara hiyo, atashirikiana na Dk Possi.
Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Mavunde alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ndipo alipoamua kugombea ubunge katika Jimbo la Dodoma Mjini ambako aliibuka mshindi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi uliomalizika Oktoba mwaka huu.
Wengine ni William ole Nasha ambaye amekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nasha ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro, alichukua nafasi hiyo baada ya kumuangusha katika kura za maoni aliyekuwa mbunge jimbo hilo, Kaika ole Telele.
Aidha, katika Wizara ya Ujenzi ambayo bado Waziri wake hajateuliwa, Dk Magufuli amemteua Mhandisi Edwin Ngonyani kuwa Naibu Waziri. Kabla ya kuwania ubunge na kushinda Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Ngonyani alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Katika Wizara ya Fedha na Mipango, Naibu Waziri mpya aliyeteuliwa ni Dk Ashantu Kijaji ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini. Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Dk Issack Kamwela wa Viti Maalumu na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Dk Magufuli pia katika baraza lake hilo, amemteua Waziri mpya, Dk Hamisi Kigwangallah ambaye ni Mbunge wa Nzega kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mwingine ni Mbunge wa Chato, Dk Merdad Kalemani kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Waziri huyo alishinda katika jimbo hilo ambalo lilikuwa ndio jimbo la Rais Magufuli katika Serikali ya Awamu Nne. Alikuwa mfanyakazi wa wizara hiyo kabla ya kujitosa kuwania ubunge mwaka huu. Kwa upande wake, Mbunge wa Katavi, Dk Issack Kamwela ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Kabla ya kuwa mbunge, Kamwela alikuwa Mhandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kabla ya kugombea Katavi ambako amechukua nafasi ya ubunge ya Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda.


Post a Comment

 
Top