0
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilijadili ajenda ya Afya na Sera ya Mambo ya Nje ambapo pamoja na mambo mengine lilipitisha azimio linalotathmini utay
ari wa nchi wanachama kukabiliana na magonjwa ya milipuko na dharura nyingine za kiafya.

Katika mjadala huo, wazungumzaji wengi, walisisitiza   umuhimu wa kuimarishwa kwa mifumo ya afya, hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati zisizo na uwezo wa kutosha wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko. Wazungumzaji hao walieleza umuhimu wa kung’amua mafunzo muhimu ya janga la ugonjwa wa Ebola uliosababisha maafa makubwa katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Akichangia katika mjadala huo kwa niaba ya serikali ya Tanzania, Bw. Noel Kaganda, Afisa Mwandamizi katika Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa alisema kuwa pamoja na jitihada zilizolenga kuimarisha sekta ya afya katika kipindi kilichomalizika cha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile upungufu wa madaktari na wauguzi; vifaa finyu na vichakavu; na mazingira yasiyo salama.

Aksisitiza  kuwa, jitihada za kuboresha afya ya binadamu, hususan ya akina mama na watoto, lazima ziendelezwe kwa ufanisi zaidi katika muktadha wa Agenda ya Maendeleo Endelevu  hadi kufikia mwaka 2030.

Aliongeza kuwa pamoja na kuzuia vifo vya watoto wachanga, ambavyo idadi yake ulimwenguni kwa mwaka 2015 imefikia milioni 6, sawa na vifo 16,000, jumuiya ya kimataifa haina budi kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile Ebola na mengineyo, ambayo yanaweza kuathiri jamii nyingi duniani kufuatia kushamiri kwa utandawazi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na binadamu.

Pamoja na kusisitiza kuwa wananchi wote wapatiwe huduma bora za afya, Tanzania iliunga mkono mapendekezo ya ripoti ya wa Shirika la Afya Duniani kuhusu ulinzi na ustawi wa watumishi katika sekta ya afya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watumishi wengi wa sekta ya afya wanadhalilishwa na kushambuliwa wakiwa kazini na wanaathirika na majanga mengine kama vile Tsunami na matetemeko ya ardhi. Tanzania ilisema kuwa vitendo hivyo vinachangia katika kuzorota kwa sekta ya afya, hivyo ilitaka vikomeshwe mara moja. Pia ilipendekeza wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Vilevile ilitaka watumishi wa sekta ya afya wapatiwe mafunzo na zana za kujilinda na maambukizi, ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo. Kadhalika ilisisitiza umuhimu wa mashirikiano baina ya nchi wanachama na wadau wengine wa afya, kama vile Shirika la Afya Duniani, yenye lengo la kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani imekuja siku chache kabla ya jopo la Ngazi ya Juu lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupendekeza namna bora ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko duniani. Jopo hilo linaloongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, linatarajia kuwasilisha taarifa yake mwezi Januari 2016.

Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeazimia kufanya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu “antimicrobial resistance” kwa lengo la kubaini kiini cha magonjwa sugu kama kama ilivyo kwa baadhi ya jamii za ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Post a Comment

 
Top