HALI ELIMU IMETOA RIPOTI YA UTEKELEZAJI WA AHADI ZA KIKWETE KATIKA ELIMU NA UDHAIFU WAAKE Katika
ripoti hiyo ambayo iliandaliwa na jopo la wataalamu na wadau wa elimu
mbalimbali ambao walifanya katika mwezi Julai na Agosti mwaka huu, pia imebaini
utekelezaji hafifu wa ahadi zake alizokuwa
akizitoa kwenye sera zake kuhusu
uboreshaji wa sekta ya elimu.
Akichambua ripoti hiyo baada ya kuzinduliwa na Mwenyekiti wa
Bodi HakiElimu, Martha Qorro, Mhadhili wa Chuo Kikuu Dar es Salaam Prof. Kitila
Mkumbo amesema, katika utafiti huo pia walibaini kuwa, Rais Kikwete hakuongeza
vitu vipya katika uongozi wake kuhusu sekta ya elimu bali aliendeleza yale
aliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Hakuwa na falsafa mpya katika sekta ya elimu bali alichokuwa
anafanya ni kuyabeba kila anayoyapata kama yalivyo na kuanza kufanyia kazi.
“Mfano; alisema ataanzisha shule za kimataifa nchini lakini hizo
hizo alizoziongeza ndio zipo hoi, hadi sasa shule zenye viwango vinavyokubalika
nchini ni asilimia nne tu,” amesema Mkumbo.
Mkumbo amesema, alichofanikiwa Rais Kikwete katika uongozi wake
ni kupanua fursa za elimu ambapo aliweza kuongeza miundombinu kwa kuongeza
madarasa, matundu ya vyoo, kuongeza idadi ya walimu, vitabu, udahili, uwiano
kati ya wasichana na wavulana wanaojiunga na shule ya msingi na sekondari
lakini sio katika suala la ubora wa elimu.
“Mathalani, shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka
2005 hadi 16,538 mwaka 2015 huku wanafunzi wa shule za msingi wakiongezeka
kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892, shule za sekondari zimeongezeka kutoka 1,745
mwaka 2005 hadi 4,753 mwaka 2015 huku idadi ya wanafunzi shule za sekondari
zikiongezeka 524,325 mwaka 2001 hadi 1,804,056 mwaka 2015.
“Vyuo vya ufundi pia vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744
mwaka 2015 huku idadi ya wanafunzi katika vyuo ikiongezeka kutoka 40,059 hadi
145,511 mwaka 2015. Licha ya wanafunzi kuonekana kuwa wengi shuleni na vyuoni,
tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonesha wanafunzi wengi hawajui kusoma wala
kuandika,” amesema Mkumbo.
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage akisoma
mapendekezo yaliyopo kwenye ripoti hiyo amesema kuwa, serikali iliyopo
madarakani hivi sasa inatakiwa kuchukua maoni yaliyopendekezwa kwenye ripoti
hiyo na kuyafanyia kazi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akitaja baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo Kalage
amesema, serikali ya Awamu ya Tano inatakiwa iwatazeme walimu kwa jicho
lingine.
Ili elimu iwe bora lazima walimu pia wawe bora na sio bora
walimu hivyo iunde bodi ya kuwachunguza walimu labla ya kuanza kazi kama ilivyo
kwa madaktari baada ya kumaliza masomo.
Amesema mapendekezo mengine ni kuwajali walimu ili wapate moyo
wa kufanya kazi hiyo kwa kuwajengea nyumba kwani ni asilimia 22 tu ya walimu
ndio wamepewa nyumba na kuboresha mioundombinu katika mazingira wanayoishi.
Kuboresha madarasa, vifaa vya kufundishia, ukaguzi kwa walimu na mazingira ya
shule yaimarishwe.
“Ni kazi ya Rais John Magufuli sasa kuiboresha sekta ya elimu
kwani hiyo ndio sekta muhimu na kubwa kuliko zote na ndiyo yenye bajeti kubwa
kuliko zote lakini utendaji wake ni ziro sasa hiyo bajeti inaendaga wapi?
“Walimu mishahara haiboreshwi, wanafunzi wengi hawajui kusoma
wanamaliza shule kichwani hakuna kitu,” amesema Kalage
Post a Comment