Wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli, pamoja na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameshindwa kushiriki mdahalo maalum wa wagombea urais ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza pamoja na wadau wengine.
Mdahalo huo ambao umefanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo, ulirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star TV. Anna Mghwira kutoka Chama cha ACT-Wazalendo na Chief Lutasola Yemba wa ADC na mgombea kutoka CHAUMMA, Hashim Rungwe ndiyo wagombea pekee wa urais waliopewa mualiko rasmi na kushiriki mdahalo huo.
Hata hivyo, Rungwe alifika wakati mdahalo huo ukiwa unaelekea ukingoni ambapo awali ilitaarifiwa kuwa angefika kwa kuchelewa kwa kuwa wakati mdahalo umeanza yeye ndio alikuwa akiwasili Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere akitokea Mtwara.
Katika mdahalo huo, maswali mbalimbali yaliulizwa ikiwemo dhana nzima ya mabadiliko ambayo awali ilikuwa ikitumiwa na Chadema kisha kuenea kwenye vyama vingine, imepata tafsiri tofauti kutoka kwa wagombea urais wa ACT-Wazalendo Anna Mghwira na Chief Yemba wa ADC.
Kwa mujibu wa Mghwira, dhana ya mabadiliko katika ACT-Wazalendo ni hoja mbadala inayolenga kushughulikia matatizo ya jamii. Alisema ACT-Wazalendo imebuni mikakati madhubuti wa kuongeza uzalishaji kupitia rasilimali za nchi kama vile misitu, madini na uwekezaji kwenye kilimo.
“Matumizi bora ya rasilimali na uwekezaji katika kilimo vitasaidia kuongeza pato la taifa na hivyo itarahisisha utoaji wa huduma bora za jamii kama vile elimu na afya,” alisema Mghwira.
Kwa upande wake, Chief Yemba alisema dhana ya mabadiliko kwa mujibu wa ADC ni kuondoa maradhi, ujinga na umasikini. Alisema mabadiliko siyo kuiondoa CCM madarakani na kisha kuiongoza nchi kwa misingi ileile ya CCM.
Kuhusu Muungano, Chief Yemba alisema ADC itapitia kero zote ili Muungano uweze kutoa haki sawa kwa watu wote tofauti na ilivyo sasa. Alisema Muungano unapaswa kusimamia na kutekeleza hoja ya haki sawa kwa wote kama vile kutoa huduma za jamii kwa usawa kwa pande zote za Muungano.
“Sisi ACT-Wazalendo tunasema Muungano ni lazima utokane na ridhaa ya wananchi kikatiba tofauti na ilivyo sasa. Hoja za wananchi kudai serikali ya Tanganyika au Zanzibar yenye mamlaka kamili, zinaonyesha wazi kwamba Muungano tulionao unahitaji marekebisho ili wananchi wenyewe waridhie,” alisema Mghwira.
Mgombea urais kupitia Chama cha TLP, Maxmilian Lyimo, pamoja na kwamba hakuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye mdahalo huo, alipata fursa ya kujibu baadhi ya hoja za wananchi kama vile afya bora. Alisema serikali yake haitafanya dawa kweye hospitali za umma kuwa bidhaa adimu kama ilivyo sasa.
Post a Comment