Tume ya Utangazaji Zanzibar, imetoa onyo kwa wamiliki wa vyombo vya
habari ikivitaka kutokimbilia kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya kut
olewa
rasmi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Chande Omar alitoa onyo hilo
alipokuwa akizungumza na wamiliki wa vyombo vya habari katika mkutano wake
uliofanyika Wizara ya Habari, akikumbusha kosa lililofanyika katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana na chombo kimoja cha habari kufungiwa kwa
kutangaza matokeo kabla ya wakati.
Aliwataka wamiliki na wahariri wa vyombo hivyo kuhakikisha
wanafuata maadili ya uandishi wa habari na kuzingatia taratibu na sheria za
nchi katika kutangaza na kuandika mambo yanayohusu uchaguzi.
Alisema iwapo chombo chochote cha habari kitakwenda kinyume na
sheria na kutangaza matokeo ya uchaguzi, hakitovumiliwa, kitafungiwa na kutozwa
faini.
“Chombo chochote cha habari kinapoomba usajili kinapewa sheria na
kanuni ambazo ni mwongozo wa utendaji kazi, kwa hivyo kama kimekubaliana na
mwongozo huo wakija wakakiuka, watakuwa wamevunja sheria na tume haitavumilia,
kitafungwa na kitatozwa fidia,” alisema Omar.
Aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuwahabarisha
wananchi ikiwamo kutopendelea upande mmoja katika kuripoti matukio ya uchaguzi
na kuwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu ili nchi ibaki
salama.
Mkurugenzi wa Sahiba FM, Maalim Kassim Suleiman alisema walifungiwa
kwa kosa hilo lakini walifunguliwa baadaye na wanaendelea kurusha matangazo
kama kawaida.
“Hasara ilikuwa kwa wasikilizaji wetu wakati hatukuwepo hewani na
hili ni tatizo kubwa, lakini tunaamini kasoro kama hizo hazitafanyika tena kwa
kuwa lengo letu ni kufanya kazi kwa kufuata maadili na miongozo iliyowekwa,”
alisema mkurugenzi huyo ambaye aliwahi kuwa mtendaji wa Serikali ya Zanzibar.
Kituo hicho kilifungiwa Oktoba 28 mwaka jana na kufungiliwa Januari 13.
Post a Comment