Hamidu Bobali ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mchinga na Mwenyekiti wa JUVICUF amezungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CUF jijini Dar es Salaamamedai kuwa ulipuaji huo unafanywa na baadhi ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“CCM kwa kushirikiana na vyombo vya usalama imekuwa ikijaribu
kuficha ukweli kuhusiana na Zanzibar. Kumekuwa na ulipuaji mabomu unaoendelea visiwani humo, ambapo ukichunguza utaona mabomu yanayolipuliwa ni ambayo mwananchi wa kawaida hawezi kumiliki,” amesema.
“Hata siku moja sijawahi sikia kuna nyumba imelipuliwa ambayo haikuwa na watu ndani yake, nyumba zote zilizodaiwa kulipuliwa na wanachama wa CUF hakukuwa na watu ndani yake,” ameongeza Bobali.
Bobali amehoji “Kama kweli wanaolipua mabomu hayo wangekuwa walipuaji kweli, wanheleta madhara makubwa, lakini cha kushangaza mabomu hayakuwadhuru watu.”
Bobali amesema kuwa, nyumba iliyolipuliwa maeneo ya Kisonge visiwani Pemba hivi karibuni, haikuwa na watu ndani yake wakati bomu lilipolipuliwa, pia amesema kwenye nyumba ya Kamishna wa Polisi ambayo ililipuliwa hakukuwa na mtu wakati wa utekelezaji wa tukio hilo.
“Matukio hayo mawili yanadhihirisha kwamba mashambulizi yalipangwa, na kwa sababu Pemba kuna wananchama wengi wa CUF wameona bora wawatupie lawama ili mwisho wa siku wakichafue chama na kuwafanya wanachama kuonekana waanzilishi wa machafuko,” amesema.
Amesema, kinachoendelea Zanzibar ni utumiaji mbovu wa vyombo vya dola pamoja na Jeshi la Polisi kuvaa vazi la ukada jambo linalopelekea kusahau majukumu yao ya kuwalinda wananchi pasipo kuangalia itikadi zao za vyama.
“Tumeshuhudia watu wakipigwa lakini polisi hawakuchukua hatua yeyote, pia tumemsikia na kushuhudia mwenyekiti wa UVCCM Sadifa Juma akiandika maneno yanayolenga uchochezi lakini hadi leo anaachwa akitamba uraiani,” amesema.
Bobali amesema, Sadifa aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook maneno yasemayo “Vijana wa CCM tumechoka kuchokozwa na JUVICUF,” ambapo aliamuru vijana wa CCM kuwashughulikia vijana wa CUF.
“Hivi karibuni nilikutana na Sadifa, nikamhoji juu ya kauli aliyoiandika ili nijue kama alidhamiria au la, lakini alinithibitishia kuwa alidhamiria kile alichokiandika kwamba kitekelezwe,” amesema.
Mahmoud Mahinda, Katibu Mtendaji wa JUVICUF Taifa, amesema matukio yanayoendelea kufanyika Zanzibar yanafaywa kwa msaada wa CCM na kufafanua juu ya kundi la Mazombi ambapo alidai kuwa ni vijana wa CCM waliowekwa katika makambi.
Aidha, JUVICUF imeshangazwa na mkanganyiko wa viongozi visiwani humo ambapo Mkuu wa Mkoa wa Pemba Kaskazini aliashiria hali ya hatari na kuamuru wananchi kujifungia ndani inapojiri majira ya saa mbili usiku.
Taarifa hizo zinakuja wakati Charles Kitwanga, Waziri wa Mambo ya Ndani ameshasemakuwa hali Zanzibar ni shwari na ulinzi uliohimarishwa na kutaka kuwahakikishia wananchi usalama ili wajitokeze kupiga kura kwenye uchaguzi wa marudio.
Post a Comment