Jopo la Madaktari wanaomtibu Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania,
Abubakar Zubeir wamezuia kwa muda watu
kwenda kumtembelea kiongozi
huyo wa dini ili apate muda zaidi wa kupumzika.
Akizungumza na Mwananchi jana jioni, Daktari wake, Profesa Mohamed
Janabi alisema: “Tumewaomba Mufti aachwe kwa muda ili apumzike. Mimi, Dk
Mwanga, Dk Othman na Dk Abel tumeshauri leo (jana) apumzike na kupewa mazoezi
zaidi maana watu wa madhehebu yote wamekuwa wengi mno.”
Hatua hiyo ya Dk Janabi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikolazwa Mufti Zubeir, iliwafanya viongozi
mbalimbali wa dini akiwamo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum,
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima pamoja na Mbunge wa
Kinondoni Mussa Mtulia kushindwa kumwona jana.
Viongozi hao waliowasili katika taasisi hiyo ya Muhimbili saa kumi
na moja jioni, walitumia saa nzima kusubiri kama watapata ruhusa ya kumuona
Mufti bila mafanikio.
“Nimekuja hapa kumuona Mufti Zubeir kama kiongozi mwenzangu wa
kidini, tunamwombea heri apate ahueni,” alisema Askofu Gwajima ambaye baadaye
aliamua kuondoka.
Mtulia alisema baada ya kufika hospitalini hapo wamekuta maelekezo
kwamba daktari wake ameomba apumzishwe, daktari anataka apone haraka kwani
wageni wamekuwa wengi.
“Nilikuja kumwona Sheikh Zubeir baada ya kufika nimeshindwa kumuona
baada ya daktari wake kuomba aachwe apumzike, tunaamini tutapata muda wa
kumuona baadaye Jumamosi,” alisema Mtulia.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Sheikh
Suleiman Lolila alisema jana kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo na watu
wengi, ndugu, jamaa na marafiki wanaotaka kumjulia hali na kumfanya akose muda
wa kupumzika.
“Hali ya Mufti inaendelea vizuri, tunajua Mufti ni mtu wa watu,
lakini tunataka apate muda zaidi wa kupumzika, tunachofanya ni kudhibiti wingi
wa watu,” alisema Sheikh Lolila.
Post a Comment