0

Kazi za usafi wa mazingira kwenye maeneo tofauti Nchini katika kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeonekana kuitikiwa vyema na Wananchi walio wengi pa
moja na vikosi vya ulinzi hapa Nchini. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alijumuika na Wananchi hao kwa kazi za usafishaji wa Mtaro wa maji machafu unaokusanya maji kutokea mitaa ya Muembe Njugu, Kwahani, Kariakoo, Kilimani na Kumalizikia Pwani ya Kilimani. 
Akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Nd. Mzee Khamis alisema Baraza la Manispaa limeanzisha mradi maalum wa usafi wa mazingira katika Manispaa ya Zanzibar kwa kuwashirikisha moja kwa Wananchi kwenye Mitaa yao. Mhandisi Mzee alisema hatua hiyo itatoa fursa pana kwa kila mwananchi kuona kwamba suala la usafi wa mazingira ambalo linapaswa kuwa la kudumu linaigusa Jamii moja kwa moja badala ya kufikiria kuwa jukumu hilo ni la Baraza la Manispaa pekee. 
Akizungumza na washiriki wa zoezi hilo la usafi wa mazingira kwa ajili ya kuanza kwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 52 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Wananchi pamoja na Vikosi vya ulinzi kwa ushiriki wao wa usafi wa mazingira. 
Katika kazi hiyo ya usafi wa mazingira kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi ya vifaa tofauti vya usafi wa mazingira kwa Kikundi cha usafi wa Mazingira cha Kilimani City. 

Vifaa hivyo vyenye Thamani ya Shilingi Laki Saba vimetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Idara yake ya Mazingira ikiwa ni muendelezo wa utaratibu iliyojipangia wa kutoa zawadi za vifaa kila mwaka kwa Vikundi vilivyoonyesha juhudi katika kushiriki kwenye usafi wa mazingira maeneo mbali mbali Nchini.

Post a Comment

 
Top