0
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema operesheni kwa lengo la kuwachukulia hatua raia wa nje wanaofanya kazi nchini bila kufuata sheria za nchi, ni endelevu na itagusa maeneo yote ikiwemo wafanyakazi wa majumbani.

Msemaji wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, jana alisema hawakukurupuka kuendesha operesheni hiyo, bali hakuna mgeni anayeruhusiwa kufanya kazi nchini bila vibali.

Tamko hilo la kusisitiza limekuja huku takwimu zikionesha kwamba, hadi mwishoni mwa wiki, watu 79 walishakamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma nazo.

“Lengo la Wizara ni kuhakikisha operesheni hii inaenda kwa kasi na kwa ufanisi, tutagusa maeneo yote, iwe viwandani, mashambani na hata majumbani lazima lengo letu litimie,” alisema Nantanga.

Alisisitiza, “Nawatahadharisha wale wote wanaodai kuwa tumekurupuka, watambue kuwa hakuna mgeni yeyote anayeruhusiwa kufanya kazi nchini kinyume cha Sheria, hivyo wale wote wanaoendelea kuwaajiri wageni wa aina hiyo wamevunja Sheria.”

Alisema Serikali inafanya kazi kuhakikisha nchi inakuwa salama na watu wote wanafuata Sheria. Alisema kuendelea kuwepo kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi bila vibali ni kuvunja Sheria.

Aliwataka raia wa kigeni wanaotambua kuwa wanafanyakazi kinyume cha sheria, ikiwemo kutokuwa na vibali, kujisalimisha wenyewe ofisi za Uhamiaji kabla ya kufikiwa na operesheni hiyo.

Aidha aliwataka waajiri wote kuhakikisha raia wote wa kigeni waliowaajiri wanafanya kazi kihalali. Alisisitiza, endapo kuna raia wa kigeni asiye na kibali au yuko kinyume cha Sheria, asalimishwe Uhamiaji mara moja kabla sheria haijachukua mkondo wake, au kuwasili sha taarifa zake.

Alitoa mwito kwa wananchi wenye taarifa za kuwepo kwa raia wa kigeni, wanaoishi au kufanyakazi kinyume cha sheria, kuziwasilisha wizarani ziweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

“Natoa onyo, watu wasije wakajificha na kudhani kuwa wako salama kwa sababu operesheni hii ni endelevu, popote walipo tutawafikia,”alisema. 

Hadi mwishoni mwa wiki watu 79 walishakamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma nazo.

Post a Comment

 
Top