Jeshi la Polisi
limemkamata raia wa Nigeria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere
(JNIA), kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya ambazo thamani yake ni kubwa
ingawa haijajulikana.
Kamanda wa
polisi wa JNIA, Martin Ottieno alisema
mtuhumiwa huyo, Ejiofor Ohagwu (33), alikamatwa na kilo nne za dawa hizo ambazo
alisema licha ya kutofahamu thamani yake kwa sasa, inaweza kuwa kubwa kwa
sababu hawajawahi kukamata dawa za kiwango hicho.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, kilo moja
ya heroin kwa bei ya mitaani ni kuanzia Sh90 milioni.
Ottieno alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa saa
8:00 usiku wa kuamkia jana kwenye sehemu ya ukaguzi ya eneo la wasafiri
wanaoondoka.
Alisema awali polisi walipata taarifa za
kiintelijensia kuhusu Ohagwu na alipopekuliwa alikutwa na dawa alizodai kuwa ni
heroin zilizofungwa katika pakiti sita za plastiki.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa anasafiri kuelekea mji wa
Lagos, Nigeria, akitumia Shirika la Ndege la Ethiopia,” alisema.
“Dawa hizi alizificha kitaalamu kwa kushonea
pakiti zote pembeni mwa mabegi yake mawili ya nguo ili asibainike haraka na
vyombo vya dola.”
Alisema polisi bado inamshikilia mtuhumiwa huyo
na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Pia, alisisitiza kuwa kwa sasa viwanja vya ndege
si vichochoro vya kupitisha dawa hizo, kwa kuwa polisi ikishirikiana na wadau
wengine, imejipanga kupambana na aina hiyo ya uhalifu.
“Mbali na kuwakamata hawa, pia tumelenga
kuwakamata mapapa wanaoagiza dawa hizi, ” alisema Kamanda Ottieno.
Desemba 17 mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga alikutana na maofisa wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam na
kutaka wamueleze mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya.
Hili ni tukio la kwanza kutokea tangu mwaka
uanze.
SOURCE MWANANCHI
Post a Comment