Membe
amepinga uamuzi wa kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi visiwani Zanzibar
akisema dunia inashangaa, na akaitaka CCM na Serikali isiwaachie watu wawili tu
kutafuta njia za kutatua m
gogoro huo.
Membe
anakuwa mwanasiasa wa kwanza mwandamizi kutoka chama tawala kuonyesha waziwazi
kutoridhishwa na uamuzi wa kufuta uchaguzi huo wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi
na madiwani ambao ulifanyika sambamba na uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano,
wabunge na madiwani wa Bara na Visiwani.
“Kinachoishangaza
dunia si kuahirisha uchaguzi, bali ni kufuta matokeo ya majimbo yote,” alisema
mwanadiplomasia huyo katika mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti hili
mapema wiki hii.
Uchaguzi
wa viongozi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 sambamba na Uchaguzi Mkuu,
ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha Oktoba 28
kwa maelezo kuwa sheria na taratibu zilikiukwa na akaahidi kuitisha uchaguzi
mwingine baada ya siku 90 zinazomalizika wiki ijayo.
Chama
kikuu cha upinzani visiwani, CUF, ambacho kilimsimamisha Maalim Seif Sharif
Hamad kugombea urais, kinapinga uamuzi huo kikisema si mwenyekiti wa tume wala
ZEC wenye mamlaka ya kufuta matokeo na kutaka mshindi atangazwe ili chama hicho
kwa kushirikiana na CCM vikutane kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Katika
kujaribu kutatua mgogoro huo, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Maalim
Seif wameshafanya vikao tisa Ikulu Zanzibar pamoja na marais wa zamani wa
visiwa hivyo, Dk Amani Karume, Dk Salmin Amour na Ali Hassan Mwinyi, bila ya
mafanikio na tayari katibu huyo mkuu wa CUF ameshatangaza kujitoa kwenye
mazungumzo hayo.
Akizungumza
kuhusu mgogoro wa kisiasa visiwani, Membe alisema inashangaza kuona uchaguzi
ulifutwa kwenye majimbo yote, badala ya yale yaliyokuwa na matatizo.
“Kilichotokea
Zanzibar kimeihuzunisha dunia,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Mtama
mkoani Lindi. “Watanzania waelewe, kilichoishitua dunia ni kule kufuta matokeo
kwa ujumla wake. Yaani majimbo yote hakuna hata moja lililofanya vizuri? Hapa
ndipo tunapata kigugumizi. Sasa tunakwenda wapi, tunafanya kitu gani?
“Ilitakiwa
kuwe na ubaguzi; majimbo mawili, matatu, manne, matano, haya hayajafanya vizuri
ndiyo uchaguzi urudiwe. Kaubaguzi kale kangewekwa, hiyo ingefanana na sura ya
dunia ya haki.”
Waziri
huyo mstaafu aliyehudumu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa
miaka tisa, pia haridhishwi na jinsi mgogoro huo wa kisiasa unavyotafutiwa
ufumbuzi kutokana na kuwahusisha zaidi Dk Shein na Maalim Seif.
“Kama kuna
mwanasiasa anadhani tatizo la Zanzibar litamalizwa na sehemu moja ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pekee, anafanya makosa makubwa,” alisema Membe.
“Umoja
wetu na Zanzibar ni umoja wa kusaidiana wakati wa raha na matatizo. Hili ni
tatizo ambalo linaweza kuhatarisha si tu usalama wa Zanzibar, bali pia Muungano
wetu. Hatuwezi kukaa tu na kuangalia.
“Chama
chetu na Serikali yetu lazima vishiriki kwa vitendo na kauli kumaliza mgogoro
wa Zanzibar na ikiwezekana wahamie huko. Hili tatizo ni kubwa.”
Membe
alisema katika mgogoro huo, Watanzania wa Bara wana haki ya kujua
kinachozungumzwa ili kushauri kwa lengo la kudumisha Muungano.
“Kuwaacha
viongozi wawili tu wanakutana kila siku kwa muda wa mwezi mzima au miezi miwili
na hujui kinachoendelea si sahihi. Huwezi kujua kinachoendelea,” alisema.
“Kuna
mambo makubwa yanayoendelea, lakini hawataki tu kutuambia. Msije mkadanganyika
kwamba wanakutana mle, wanakunywa chai, wanaondoka halafu mnasema hakuna
kinachoendelea.”
Wakati ZEC
imetangaza Machi 20 kuwa tarehe ya kurudia uchaguzi, CUF imekuwa imeshasema
kuurudia si suluhisho na haitakubalika, badala yake ameitaka Tume kutangaza
mshindi.
Membe,
ambaye alikuwa mmoja wa makada 38 wa CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya
kugombea urais lakini akaishia kwenye tano bora, alikuwa pia na maoni yake
kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi.
“Lazima
uangaliwe kwa mapana, tusiangalie kama turudie uchaguzi au tusirudie.
Tusifikiri viongozi wa Zanzibar wakikutana wanaulizana swali hilo tu
kwamba ‘turudie uchaguzi au tusirudie’. Hapana,” alisema Membe aliyeshiriki
kutatua migogoro mbalimbali barani Afrika.
“Wenzako
swali hilo ni dogo sana. Huenda wako kwenye swali kubwa. Wanaweza kuuliza swali
kama ‘hivi tatizo la Zanzibar ni kitu hiki au kuna tatizo kubwa zaidi ya hapa’.
Hivi mnaweza kukaa saa tatu au nne mkaulizana tu kwamba, ‘turudie, tusirudie,
turudie tusirudie?’”
VIPI
WALIOHAMA CCM WAKATI WA UCHAGUZI
Akijibu
swali lililotaka kujua anavyowazungumzia na kujisikia kuhusu watu hao, Membe
alisema: “Nikionana nao najisikia kichefuchefu. Tena ukiwaona waambie, chama
kichukue hatua kwa wasaliti.”
Alisema
zipo taarifa za baadhi ya waliohama CCM kutaka kurejea, akashauri kisiwapokee
tena.
SOURCE Mwananchi
Post a Comment