Dalili za mgawanyiko kwenye kamati hizo zilianza kuonekana juzi, baada ya wabunge hao wa Kambi ya Upinzani kufanya kikao na kuweka msimamo wa kutaka kushirikishwa kwenye uteuzi wa wajumbe.
Kambi ya Upinzani ilisema inataka kushirikishwa katika hatua hiyo ikidai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekuwa ikiwapangia watu wa kuongoza kamati zinazosimamia mapato ya serikali ambazo kikanuni zipo chini yao.
Viongozi hao wa kambi ya upinzani walidai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipangiwa watu wa kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali za (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambazo kikanuni zinatakiwa kuongozwa na upinzani.
Baada ya Ofisi ya Bunge kutangaza majina ya wajumbe wa kamati, Kambi ya Upinzani Bungeni ilikutana na waandishi wa habari, lakini wakaahirisha kwa madai kuwa wamegundua kwamba orodha ya majina yaliyotoka, yana matatizo mengi zaidi.
“Tumegundua kwamba matatizo hayapo kwenye kamati ya PAC na LAAC tu, kwenye kamati nyingi kuna matatizo kwa hiyo kwa sasa viongozi wa kambi wanakutana kujadili na kuchambua taarifa iliyotolewa baadaye tutakutana na wabunge wote kisha kesho tutatoa msimamo wetu,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika.
Baada ya kauli hiyo, Mnyika aliulizwa inakuwaje wao wanaendelea na vikao wakati wenzao wa CCM wakiwa kwenye uchaguzi:
“Siwezi kujibu chochote, neno lolote nitakalosema, nitaingilia hicho kinachojadiliwa na viongozi. Wewe subiri kwanza tumalize kikao, tutoke na msimamo wa pamoja na kesho tutawaeleza msimamo wetu,”alisema Mnyika.
Awali, kabla ya kutolewa kwa majina hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema kwa muda sasa wamekuwa wakichaguliwa watu wa kuongoza kamati hizo na CCM.
“Ni sawa na mtu anakupa kitu kwa mkono wa kushoto na kukunyang'anya kwa mkono wa kulia. Ndiyo maana tukataka tushirikishwe kuanzia wajumbe watakaokuwa kwenye kamati hizo,”alisema Sakaya ambaye ni Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora.
Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili 2013, inasema:“Wenyeviti wa Kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hizo ambao wanatoka katika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.”
Post a Comment