Mwenyekiti wa Jopo la Ngazi ya juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya, Rais Mstaafu, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, jana Jumatatu, amemkabidhi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon, Ripoti ya Jopo lake.
Mhe. Jakaya Kikwete aliteuliwa na Ban Ki Moon, kuongoza Jopo lililokuwa na wajumbe watano mwezi Aprili 2015. kwa mujibu wa hadidu za rejea Jopo hili lilitakiwa kutekeleza majukumu yake kuanzia mwezi Mei hadi Desemba 2015.
Akipokea ripoti hiyo, katika hafla fupi iliyofanyika Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa . Ban Ki Moon, pamoja na kumshukuru Mwenyekiti wa Jopo Mhe. Jakaya Kikwete pamoja na timu yake, amesisitiza kwamba, mapendezo yaliyotolewa na Jopo hilo yatazingatiwa na kufanyiwa kazi.
“ Ninatoa shukrani zangu za pekee na za dhati kwako wewe kama Mwenyekiti kwa uongozi wako , na pia kuwashukuru wajumbe uliofanya nao kazi. Ripoti hii ambayo imesheheni mapendekezo na ushauri itazingatiwa na kufanyiwa kazi”. Amesema Ban Ki Moon
Akabanisha kwamba, mapendekeo na ushauri uliomo ndani ya Ripoti ya Jopo atauwasilisha pia kwa Shirika la Afya Duniani ( WHO).
Katibu Mkuu pia amesema Ripoti hiyo itasaidia sana katika kutoa mwongozo kwa Jumuiya ya Kimataifa juu ya namna ya kuimarisha na kuboresha miundombinu ya afya ili iweze kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemhakikishia Mwenyekiti wa Jopo Mhe. Jakaya Kikwete na wajumbe wake kwamba, Ripoti hiyo itawekwa hadharani mapema iwezekanavyo ili Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na makundi mbalimbali ya jamii waweze kuisoma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jopo, Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, amemshukuru Katibu Mkuu Ban Ki Moon, kwa kumpatia heshima ya kuongoza Jopo hilo, jopo ambalo amesema walifanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu.
Wajumbe wengine wa Jopo hilo walikuwa ni Bw. Celso Amorim ( Brazil), Micheline Calmy ( Switzerland), Marty Natalegawa ( Indonesia) Joy Phumapi ( Botswana) na Rajav Shah ( USA).
Jukumu kubwa ya jopo hilo kwa mujibu wa hadidu za rejea, pamoja na mambo mengine, lilikuwa ni kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia na kukabiliana na majanga ya kiafya yakiwamo magonjwa ya mlipuko, ikiwa ni pamoja na kujifunza kuhusu mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa kufuatia kuibuka kwa janga la ugonjwa wa Ebola.
Katika utekelezaji wa majukumu yake Jopo lilikutana na kufanya majadiliano ya kina na makundi mbalimbali yakiwamo ya wataalamu, wawakilishi wa nchi tatu ambazo ziliathirika sana na ugonjwa wa Ebola ( Liberia, Siera Leone na Guinea),Mashirika ya Kimataifa na Kikanda , Taasisi za Fedha za kimataifa, wahudumu wa Afya, Wasomi , Watafiti, Sekta Binafsi na wataalam wa fani na kada mbalimbali.
Post a Comment