Katibu
Mkuu wa Uchukuzi, Dk Leonard Chamuliho ameingia ofisini kwa mara y
a kwanza jana
na kukabiliana na mgomo wa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)
wanaoshinikiza kulipwa stahiki zao.
Katika
mgomo huo ulioanza chinichini kwa zaidi ya siku mbili, wafanyakazi wa TRL
wanadai malimbikizo ya nyongeza ya mshahara kuanzia Julai hadi Novemba, 2014 na
fedha za kazi za muda wa ziada ya Novemba mwaka jana.
Kaimu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Boaz Nyakeke
alimwambia Dk Chamuliho kuwa wafanyakazi hao hawaridhishwi na utendaji wa
menejimenti hivyo ni bora akauondoa na kuweka mpya ili kuongeza ufanisi.
“Fedha za
wafanyakazi haziendi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama inavyotakiwa. Kuna
mwingiliano wa kimasilahi kati ya Kampuni ya Rasilimali za Reli (Rahco) na TRL
unaofanya mali kuharibika wakati bado zinahitajika kufanyiwa marekebisho
mbalimbali ya reli na vifaa vyetu,” alisema Nyakeke.
Dk
Chamuliho alisema kwa kuwa ilikuwa ni siku yake ya kwanza kuingia ofisini na
kukutana na madai hayo, ni vyema wampatie muda ili leo akutane na viongozi wa
wafanyakazi kutafuta suluhu jambo ambalo wafanyakazi hao walilikubali.
“Japo
nimeingia ofisini leo nimeona bora nije nisikilize masuala yenu. Madai mengine
hapa ni ya kihistoria na yapo kwenye ripoti za makabidhiano, hivyo tutayafanyia
kazi yakiwamo yale yanayotakiwa tufuate sheria,” alisema.
Jana,
wafanyakazi wa TRL waliongeza kasi ya mgomo na kuutaka uongozi wa Trawu kumleta
Dk Chamuliho katika karakana ya Kapuya Complex kusikiliza madai yao.
Katika
kushinikiza madai yao, wafanyakazi hao walilazimisha treni za abiria la Dar es
Salaam ‘Treni ya Mwakyembe,’ kusitisha huduma za jioni kwa kuchomoa baadhi ya
vifaa vinavyounganisha kichwa na mabehewa baada ya dereva wake kutaka kuanza
kazi.
Tukio hilo
lililazimu abiria waliokuwa wamepanda saa 3.50 alasiri kushuka na kudai fedha
zao huku wakilalamikia usumbufu na kupoteza muda. Utawala uliwarudishia nauli
zao.
Awali,
Meneja wa Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez alikana kuwapo wa mgomo wala mgogoro
wa aina yoyote baina ya menejimenti na wafanyakazi hao akidai kuwa yaliyokuwa
yakisemwa ni maneno tu ya viongozi wa Trawu akitumia utoaji wa huduma ya treni
ya abiria ya Dar es Salaam iliyofanya kazi asubuhi kama ushahidi wa maelezo
yake.
SOURCE MWANANCHI
Post a Comment