Wakati Baraza la Taifa la
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) likiendesha bomoabomoa katika maeneo kadhaa
jijini Dar es Salaam, Abdallah B
ulembo(Kwenye picha hapo juu), aliyekuwa meneja kampeni wa Rais John
Magufuli amepinga operesheni itakayofanyika nje ya maeneo ya Bonde la Msimbazi
na amemshauri Rais aingilie kati ili isitishwe.
Bomoabomoa hiyo,
inayolenga nyumba zilizojengwa mabondeni, kwenye fukwe za bahari, kingo za mito
na maeneo ya wazi, imekuwa ikipingwa vikali na wamiliki na wakazi wa nyumba
hizo kwa maelezo kuwa hawakupewa taarifa na hawajaandaliwa sehemu mbadala ya
kwenda.
Wakazi hao wamefikia
hatua ya kumlaumu Rais Magufuli kwa kutojitokeza na kukemea ubomoaji huo, ambao
katika baadhi ya maeneo umesimamishwa na Mahakama Kuu kwa muda.
Jana, Bulembo, ambaye pia
ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, aliiambia Mwananchi katika
mahojiano maalumu kuwa anakubaliana na bomoabomoa inayofanyika Jangwani
na maeneo hatarishi ya Bonde la Msimbazi, lakini akaitaka NEMC kuacha
kubomoa nyumba ambazo haziko kwenye bonde hilo.
Bulembo, ambaye
aliambatana na Rais Magufuli kwa siku 52 katika kampeni za urais alisema
kuwa operesheni hiyo inamjengea chuki Rais Magufuli kwa wananchi.
Bulembo, ambaye alikuwa
na mazungumzo na Rais Jumatatu wiki hii, alisema kuendelea kuwabomolea wananchi
nyumba walizokuwa wakiishi miaka mingi, ni kuvuruga imani waliyonayo kwa
kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambaye wakati wa kampeni zake
aliwaahidi neema.
Kauli hiyo imekuja wakati
takribani nyumba 16,000 zimeshawekewa alama ya kutakiwa kubomolewa na tayari
nyumba 700 zikiwa zimebomolewa jijini Dar es Salaam, hali iliyowaacha baadhi ya
wakazi wakiwa hawana sehemu za kujihifadhi, baadhi kupoteza fahamu na wengine
kufungua kesi Mahakama Kuu.
“NEMC wasiwe kama
wameshuka kutoka mbinguni na kukuta watu wamejenga mabondeni. Wasituharibie
imani ya wananchi kwa Rais,” alisema Bulembo ambaye alikuwa na Magufuli katika
kampeni za nchi nzima na kuwezesha CCM kushinda katika Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25, 2015.
“Kwani (NEMC) walikuwa
wapi siku zote mpaka wafanye shughuli hiyo sasa baada ya Rais Magufuli kuingia
madarakani? Sikubaliani na bomoabomoa hiyo isipokuwa hiyo ya Jangwani na sehemu
hatarishi za Bonde la Msimbazi.”
Kwa
nini Jangwani
Akijenga hoja yake ya
kukubaliana na ubomoaji wa nyumba za Jangwani katika Bonde la Msimbazi, Bulembo
alisema eneo hilo kwa sasa ni hatarishi, hasa kutokana na tishio la mvua za El
Nino.
“Kuna maeneo hatarishi
kama Jangwani na Bonde la Msimbazi, huko bomoabomoa hiyo iendelee,” alisema.
“Mbali na eneo la
Jangwani kuwa hatarishi kwa usalama wa watu, baadhi ya wakazi wake waliwahi
kuondolewa na kupewa viwanja eneo la Mabwepande, lakini wakaviuza na kurejea
upya.
“Lakini maeneo mengine
kama ya Ali Maua, kwa nini uwabomolee watu wakati hatujasikia wamepata mafuriko
na watu hao wako hapo kwa miaka yote?”
Bulembo alisema kuna
maeneo mengine ambayo kuna mabonde, lakini hayajawahi kuleta madhara kwa
wananchi hivyo hakuna haja ya kuwabomolea nyumba watu wa maeneo hayo wakati
wameishi kwa miaka zaidi ya 20 au 30.
“Kuna watu wamekaa mahali
kwa miaka 24 au 30 hawajawahi kupata mafuriko, hata kama wapo karibu na bonde,
lakini si eneo hatarishi kwanini wabomolewe? alihoji kiongozi huyo wa zamani wa
soka nchini.
“NEMC waache kuleta
hasira za wananchi kwa Rais wao, walikuwa wapi mpaka wanasubiri sasa,” alisema
Bulembo.
Rais
hapendi umaskini
Wakati wakazi hao
wanaobomolewa nyumba mabondeni wakidai kuwa operesheni hiyo inawaondoa kwenye
umaskini na kuwafanya mafukara, Bulembo alisema anaamini hata Rais hafurahii
kuona walalahoi wakiteseka kwa kuwa hata wakati wa kampeni alionyesha
kulisikitikia kundi hilo.
“Moja ya mambo
yaliyomsikitisha Rais wakati wa kampeni ni umaskini wa Watanzania. Alisema
anaomba kura za wanyonge na ndiyo maana aliahidi kuondoa kero mbalimbali,
ikiwamo kodi za wafanyabiashara wadogo,” alisema.
Nyumba
16,000 kubomolewa
Wakati Bulembo akisema
hayo, NEMC walikuwa wakiendelea na ubomoaji na uwekaji alama ya “X”, ikiathiri
wananchi wengi zaidi baada ya idadi ya nyumba zinazopaswa kubomolewa kufikia
zaidi ya 16,000.
Kwa wastani wa kaya moja
kuwa na watu wanne na nyumba moja kuwa na kaya kuanzia tano, ubomoaji wa nyumba
16,000 utasababisha watu 300,000 kukosa makazi, huku wanafunzi walio mwaka wa
mwisho wa elimu ya msingi na sekondari wakiathirika zaidi.
Hali hiyo imezidi kuwatia
wasiwasi wakazi hao huku wengine wakiporomosha vilio na kuzimia kutokana na
mawazo ya kukosa mbadala wa makazi.
Ofisa mwandamizi wa NEMC,
Arnold Kisiraga aliwaambia wanahabari jana kuwa kati ya nyumba 16,000 tayari
700 zilizokuwapo bonde la Mkwajuni, Hananasif na Suna zimeshabomolewa.
Kisiraga alisema huenda
idadi ya nyumba zitakazobomolewa itaongezeka kutokana na utaratibu unaoendelea
wa kubaini zilizojengwa mabondeni na kwamba leo watahamia Kigogo baada ya jana
kumaliza Ulongoni, Gongo la Mboto na Pugu Mnadani.
Kwa jana pekee,
alisema walibaini nyumba 885 zinazopaswa kubomolewa kutokana
na kujengwa katika mazingira hatarishi, ikilinganishwa na juzi wakati
walipobaini nyumba 647 zilizokuwa bonde la Mto Msimbazi--kuanzia Stakishari,
Ukonga hadi Gongo la Mboto. “Hili zoezi la uwekaji alama ni moja na lile
la ubomoaji linaloendelea Kinondoni. Ni vizuri zaidi wakaondoka wenyewe baada
ya kuwekewa alama. Huu muda wangetumia vizuri kujipanga kuondoka kwa sababu
yale ni maeneo hatarishi,” alisema Kisiraga wakati wa uwekaji alama hizo.
Kuhusu uchambuzi wa nyumba 681 zinazotakiwa kuachwa katika bomoabomoa kutokana
na zuio la Mahakama Kuu, alisema wanaendelea kuzibainisha na watakapomaliza
wataanza kuzibomoa haraka zile zisizohusika na kesi.
‘Ni
msiba mkubwa’
Wakati uwekaji alama hiyo
ukiendelea, vilio vilitanda na baadhi wakihoji tarehe rasmi ya kubolewa makazi
yao.
Yunis Amos, mkazi wa
Ulongoni aliangusha kilio baada ya kuona nyumba yake ikiwekwa alama.
“Ni msiba mkubwa sana,”
alisema Yunus huku akishika kichwa.
“Presha hapa inapanda na
kushuka. Tutaishije na watoto hawa na wengine ni yatima? Huyu Magufuli anataka
tuishije?”
Mkazi wa Bangulo,
Saida Ally yeye aliwajia juu vibarua wa NEMC wanaoweka alama hizo, akiuliza
eneo la kwenda baada ya nyumba yake kubainishwa kuwa itabomolewa.
“Wanasema nianze kutoa bati sasa, nizipeleke wapi? Wanasema utaratibu utafuata
baadaye, ni muda gani tuwe tumehama na tutahamaje? Sehemu ya kwenda sisi hatuna
labda wakibomoa tutaenda kulala kwa huyo mwenyekiti wetu wa mtaa, hakuna
namna,” alisema.
Azimia
kwa kushindwa kuhimili
Ofisa mipango miji wa
Ilala, Alfred Mbyopo alisema wananchi wengi wametaharuki baada ya nyumba zao
kuwekewa alama za kutakiwa kubomolewa na juzi kuna mkazi mmoja alizimia.
“Kuna taharuki kubwa sana
katika operesheni hiyo. Juzi kuna bibi mmoja pale Ulongoni A nasikia alizimia
kwa kushindwa kuhimili uchungu wa nyumba yake kuwekewa alama ya kubomolewa.
Lakini sisi tunawaokoa na hatari ya baadaye,” alisema Mbyopo.
‘Kidogo
leo naweza kula’
Wakati baadhi wakilia, kwa
Erasto Nyakiegi, kwa mkazi wa Mtaa wa Mwanapindi, Bangulo, mambo yalikuwa
tofauti baada ya kutoka kwenye ‘kifungo’ cha sintofahamu kutokana na nyumba
yake kukoswakoswa na alama hiyo.
“Tulikuwa tukiishi kwa
wasiwasi sana na familia yangu tukijua ni nyumba zote za mabondeni. Karibu
mwezi mzima nilikuwa sina hamu ya kula wala kulala, lakini leo naona nipo huru
zaidi kwa kuwa nyumba yangu ipo nje ya zinazotakiwa kubomolewa. Kidogo leo
naweza kula,” alisema Nyakiegi.
Hata hivyo, Mbyopo ambaye
yumo kwenye uwekaji alama hizo, alisema kuna uchimbaji mkubwa wa mchanga ambao
umesababisha Mto Msimbazi kuzidi kuliwa kingo zake na kuwaingiza baadhi ya
wananchi waliokuwa kwenye maeneo salama, kukumbwa na bomoabomoa.
SOURCE Mwananchi
Post a Comment