0
Wapiganaji wa Al-Shabab wamesema waliua wanajeshi wengi wa Kenya baada ya kuvamia kambi ya majeshi ya Muungano wa Afrika kusini mwa Somalia.

Kundi hilo la Kiislamu limesema limeteka na kudhibiti kambi hiyo mjini el-Ade na kuua wanajeshi 63 wa Kenya.
Wakazi wameambia BBC kwamba wapiganaji hao wa al-Shabab wamepandisha bendera yao katika kambi hiyo na kwamba walionyesha miili ya wanajeshi waliouawa katika barabara za mji huo.
Lakini msemaji wa majeshi ya Kenya Kanali David Obonyo amesema kambi iliyoshambuliwa si ya majeshi ya Kenya.
Badala yake, anasema kambi iliyo karibu ya wanajeshi wa Somalia ndiyo iliyovamiwa na majeshi ya Kenya yalijibu shambulio hilo.
Idadi ya waliofariki kutoka pande zote mbili bado haijabainika, Kanali Obonyo amesema kupitia taarifa.
Ameambia BBC kwamba ripoti kuwa wanajeshi wengi wameuawa ni “propaganda ya kawaida kutoka kwa al-Shabab”.
Baada ya kutokea kwa habari za shambulio hilo, Wakenya mtandaoni wameanza kutumia kitambulisha mada #IStandWithKDF kuomboleza wanajeshi waliouawa na kuonyesha uungaji mkono wao wa juhudi za jeshi Somalia

Afisa mmoja wa al-Shabab ameambia BBC kwamba wapiganaji hao walishambulia kambi hiyo baada ya sala ya asubuhi, walilipua lango la kambi kwa kutumia gari kisha wapiganaji wakaingia.
“Tulichukua udhibiti wa kambi baada ya saa moja ya mapigano makali,” amesema.
“Tulihesabu miili 63 ya Wakenya ndani ya kambi hiyo. Wanajeshi hao wengine wa Kenya walitorokea msituni na tunawawinda.”
Alisema wapiganaji hao watachukua magari 28 ya kijeshi kati ya 31 yaliyokuwa kwenye kambi hiyo pamoja na silaha zote.

Kambi mbili za kijeshi, moja ya Majeshi ya Kitaifa ya Somalia (SNA) na nyingine ya AU, zinapatikana eneo moja viungani mwa mji wa el-Ade, ambao unapatikana katika jimbo la Gedo, kilomita 380 magharibi mwa mji wa Mogadishu.
Al-Shabab walifurushwa kutoka mji mkuu Mogadishu, Agosti 2011, lakini bado wana nguvu baadhi ya maeneo ya Somalia na hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara nchini humo.


SOURCE BBC

Post a Comment

 
Top