0

Charles Kitwanga ambaye ni waziri wa mambo ya nje  ameagiza waajiri kutoa toa ajira kwa wageni ambazo kazi hizo zinaweza kufanywa na wazawa.

Pia, ameagiza maofisa wa Idara ya Uhamiaji kufanya operesheni maalumu kuwatimua raia wote wasio na vibali vya kuishi nchini ifikapo Januari 31, 2016.

Kitwanga ambaye alitembelea idara hiyo jana, alisema wizara yake kwa kushirikiana na Uhamiaji imeanzisha operesheni ya kuwakamata raia wote wa kigeni wanaoishi nchini kinyume cha sheria na kuwachukulia hatua stahiki.

Waziri huyo alisema kutokana na watu wengi kuishi nchini bila vibali, amewapa mwezi mmoja Idara ya Uhamiaji kufanya uchunguzi katika maeneo yote ya kazi na makazi, ili kuwaondoa walioingia nchini kinyemela.

“Katika operesheni hii, tutahakikisha tunawakamata wote na nimetoa maelekezo kwamba nitakuwa nikipewa ripoti kila Ijumaa kuanzia wiki ijayo, mpaka ifikapo Januari 31 tuwe tumesafisha nchi kabisa,” alisema Kitwanga.

Alisema kutokana na mpaka wa nchi kuwa mkubwa, Uhamiaji watawezeshwa ili kukabiliana na tatizo la upitishwaji wa wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali, kama ilivyoripotiwa hivi karibuni.

Pia, alitoa agizo kwa wananchi wa kawaida kuhakikisha wanatoa taarifa kuhusu wahamiaji haramu walioweka makazi katika maghala, kampuni na viwanda bubu ili kumaliza tatizo la wahamiaji haramu nchini.

Wafanyakazi wageni
Mbali na maagizo hayo, Kitwanga pia aliagiza wamiliki wa kampuni mbalimbali kuhakikisha hawatoi ajira kwa raia wa nje kwa kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.

“…Lakini kazi zote ambazo Watanzania wana utalaamu wa kuzifanya zitafanywa na wazawa na si wageni na zile ambazo inaonyesha wazi kwamba Watanzania hawana ujuzi huo, basi zifanywe na wageni,”alisema Kitwanga.

Kuhusu vibali, Waziri Kitwanga alisema hakuna raia yeyote wa kigeni atakayepata kibali cha kuishi nchini kama hajapata kibali cha kufanya kazi kama amekuja kwa ajili ya kazi. Lakini utaratibu mwingine kama mtu amekuja likizo utaendelea kama kawaida.

Kitwanga alisema kuanzia Jumatatu ijayo, viongozi wa wizara husika na uhamiaji, wakae wapange utaratibu mzuri utakaoonyesha kwamba hakuna usumbufu kwa raia wa kigeni ambaye anakuja kufanya kazi nchini kwa kuzingatia vigezo.

Pasi za kusafiria
Aidha, Waziri Kitwanga alisema mfumo wa uombaji wa pasi za kusafiria na vibali vya ukazi, hivi sasa utakamilishwa kwa njia ya Tehama.

Alisema mwombaji atatakiwa kufanyiwa mahojiano ya ana kwa ana pindi atakapokamilisha utaratibu wa kujaza na kuzilipia fomu hizo benki, na atapatiwa pasi ya kusafiria baada ya siku tatu huku kibali cha ukazi akikipata baada ya siku tano ili kupunguza urasimu.

“Tumeafikiana uboreshaji wa namna ya kufanya kazi na kwa mtazamo wa mbali,” alisema.

Post a Comment

 
Top