Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limelazimika kupiga mabomu ya machozi katika hospitali ya rufaa Bugando ili kumuokoa askari mwenzao aliyekuwa ameingia ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti Hospitalini hapo.
Askari huyo aliingia ndani baada ya mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema ) mkoa wa Geita Alphonce Mawazo kuwasili kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11.30 jioni baada ya viongozi wa Chadema na wafuasi wao kufikisha mwili wa Mawazo ambaye katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu aligombea ubunge wa jimbo la Busanda.
Aidha askari hao waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi walimkamata Mwenyekiti wa baraza la vijana Chadema taifa Patrobas Katambi kwa mahojiano zaidi.
Akiwatuliza wafuasi wa CHADEMA waliosindikiza mwili wa marehemu Mawazo hospitalini hapo, mgombea Ubunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema aliwataka wananchi hao kuwa watulivu huku akisisitiza kuwa CHADEMA hakitakubali kuendelea kuangalia wafuasi wake wakichinjwa kama kuku.
Aliwataka wananchi hao kuelekea ofisi za kanda za CHADEMA ambako ndiko msiba wa marehemu Mawazo unafanyika.
Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita Alphonce Mawazo aliuawa kinyama baada ya kushambuliwa kwa mapanga na mashoka kwenye tukio ambalo linadaiwa kuwa la uhasama wa kisiasa na baadae kufikishwa katika hospitali ya wilaya ya Geita ambapo alipoteza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi.
Post a Comment