0
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japan, zimewekeana saini mkataba wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 100, kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mgombea wa Nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameeleza kuwa fedha hizo zinatokana na msaada wa shilingi bilioni 93.438 kutoka Serikali ya Japan huku Serikali ya Tanzania ikichangia shilingi bilioni 8.26.
Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa hatua hio ya utiaji saini ni faraja kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwa kuwa mradi huo wa ujenzi wa ‘flyover’ utasaidia katika kupunguza kero ya msongamano wa magari jijini.
Aidha amesema kuwa Serikali ya Japan imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Serikali ya Tanzania, katika kuleta maendeleo kwa kufadhili miradi mbalimbali ya barabara na madaraja ikiwemo barabara ya Mwenge kwenda Tegeta, mradi uliogharimu shilingi bilioni 88, Mwenge kwenda Morocco ambayo ipo katika mkakati, pamoja na mradi wa ‘flyover’ wa Mbagala Rangi tatu kwenda Tazara.

Post a Comment

 
Top