0

Taasisi ya Twaweza, Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF) na Jukwaa la viongozi wa sekta binafsi nchini, zimeungana kuandaa mdahalo wa wagombea urais utakaofanyika Oktoba 18, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Lengo la mdahalo huo ni kutoa fursa ya kipekee kwa wananchi kuuliza maswali muhimu kwa wagombea wanaoomba ridhaa yao kuwaongoza pamoja na wagombea urais kuweka wazi ajenda zao kwa nchi ili wananchi wazipime.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema wananchi wanapewa fursa ya kuwasilisha maswali yao kwa wagombea urais kuanzia jana hadi Ijumaa kupitia barua pepe, ujumbe mfupi wa simu za mkononi, mitandao ya kijamii au kwa kupeleka katika ofisi za asasi zilizotajwa kuandaa mdahalo.
“Tumevialika vyama vyenye wagombea urais Zanzibar na Bara pamoja na wagombea ubunge wa majimbo yasiyopungua 55 kushirikisha wagombea wao wa Tanzania Bara,” alisema Eyakuze.
Aidha, alisema mpaka sasa vyama vya siasa vitano tu vimethibisha ushiriki vikiwamo vya Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo), Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Eyakuze alisema juhudi za kuwashawishi wagombea wa vyama vilivyobaki zinaendelea ili kuthibitisha ushiriki wao kwenye tukio hilo la kihistoria kwa kuwa tayari vyama vyao vimeshatumiwa barua rasmi. Alisisitiza kuwa vyama husika vimepewa fursa hiyo kuwanaonyesha wananchi viko tayari kujibu maswali ya moja kwa moja ya wapiga kura na kuonyesha serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi mkuu na chama kitakachoingia madarakani.
Aliongeza kuwa Oktoba 15, mwaka huu watakutana na wawakilishi wa vyama vishiriki kukubaliana sheria na kanuni zitakazotumika na kwamba siku itakayofuata kutahitimishwa mkutano na vyombo vya habari kutangaza sheria na kanuni hizo kwa wananchi.
Alifafanua kuwa katika midahalo iliyofanyika hivi karibuni iliyohusisha wawakilishi wa vyama, ilipata watazamaji 2,000,000 wa runinga na wasikilizaji wa redio milioni 3.9.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Ernest Sungura, alisema watatumia mbinu zote kuhakikisha mdahalo unafanyika kwani muda mrefu wananchi wamekuwa wakiuhitaji.
“Kila wakati tukipita mitaani watu wanatuuliza kwa nini hatuandai mdahalo,” alisema Sungura.
Sungura alisema katika kuhakikisha tasnia ya habari inafuatilia uwajibikaji TMF, itafuatilia ahadi zitakazotolewa na kushindwa kutekelezwa na wagombea kwa kutoa fursa waandishi wa habari kuzifanyia kazi.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Compass Communication, Maria Sarungi, alisema maandalizi yamekamilika na kuwahakikishia kila mgombea atakayeshiriki atapewa fursa ya kunadi sera na kujibu maswali.
Chanzo: NIPASHE

Post a Comment

 
Top