CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepanga kumshitaki mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli kwa madai ya kutumia vibaya nembo za chama hicho.
Ni baada ya Dk. Magufuli kutangaza kuwa nembo ya Movement for Change (M4C) ni Magufuli For Change wakati akifanya mkutano wake wa kampeni mkoani Kigoma kwenye Uwanja wa Kawawa uliopo Ujiji.
Katika mkutano huo Dk. Magufuli alisema “hawa jamaa zangu wa Chadema wananipenda, hata ile nembo yao ya M4C ni Magufuli for Change-maana yake Magufuli kwa Mabadiliko.”
Chadema wanaratajia kufungua kesi hiyo Septemba 21 mwaka huu na kwamba, madai hayo yatakwenda sambamba na madai ya kutumia kauli mbiu ya ‘mabadiliko Lowassa’ ambayo kaibadilisha na kuwa‘mabadiliko Magufuli’.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Ngome Kawe, Mwanasheria wa Chadema, John Malya alisema “CCM imekuwa ikivunja sheria za uchaguzi kila siku bila kuchukuliwa hatua yoyote na mamlaka husika, wanatumia nembo za Chadema ambazo zimesajiliwa na kujulikana.”
Hata hivyo imeelezwa, baada ya Dk. Magufuli ‘kuiba’ alama hizo za Chadema; wafuasi wake, bodi ya wadhamini na watu wake wa kampeni walianza kusambaza mitandaoni nembo ya M4C huku wakidai ni nembo mpya ya CCM.
Malya alisema mbali na hilo la kuiba nembo ya chama, wamekuwa na tabia ya ‘kukopi’ na ‘kupesti’ kila hatua inayo pigwa na Chadema na kuzitumia katika kampeni zao.
Akivitaja baadhi ya vitu vinavyokopiwa na CCM amesema, Magufuli amesikika mara kadhaa akiwa anatumia sera na Ilani ya Chadema na Ukawa, pia amekuwa akiiba kauli mbiu za Chadema pindi anapokuwa katika kampeni zake.
“Hii ni dalili za kushindwa kwa CCM hana sera wameishiwa na ndio maana wanafuata nyayo zetu kila tunapoenda na kila tunalofanya wanalifuatilia na kuaza kutukopi. Kwa mfano sisi tunatumia Lowassa mabadiliko mabadiliko Lowassa na wao wameshaiga kwa kutumia jina la Magufuli”.
Aidha, Malya alisema Chadema inasikitushwa sana na kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuwa kimya huku vitendo vya rushwa vinazidi kukithiri toka kwa CCM.
Malya alitaja baadhi ya matukio yenye viashiria vya rushwa kuwa, Magufuli alionenekana akimpatia mtoto pesa taslimu elfu 30000 katika moja ya kampeni zake, huku Mgombea mwenza wa CCM Samia Suluhu Hassani naye mara kadhaa ameonekana akigawa pesa kwa wananchi wanaohudhulia katika kampeni zake.
“Matukio yote hayo bado tume imekaa kimya japo kuwa tumeshapeleka barua za malalamiko na kutuahidi kulishughulikia kesho. Vivyo hivyo kwa Taasisi ya Kushuhulikia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) ambayo tulitegemea itakuwa ya kwanza kukemea hilo lakini ipo kimya na tumeshaandika barua ya malalmiko”.
Alidai, pia CCM wamezidi kukiuka sheria za uchaguzi kwa kuyachana mabango ya Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa hadharani na kwamba, wanakiuka sheria
Alisema, matendo hayo yote yanayofanywa na CCM yanakuika sheria za umiliki wa nembo za biashara ya mwaka 1986 na kanuni ya umiliki huo ya 2000 pamoja na taratibu zingine za umiliki.
Post a Comment