Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba ambaye alihamia Chadema hivi karibuni ameamua kurejea katika chama chake cha zamani kwa madai alikosea njia.
Nkumba ambaye alihamia Chadema baada ya kushindwa katika kura za maoni kugombea ubunge Sikonge, aliteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya Chadema lakini wanachama wa chama hicho walipinga kitendo cha Kamati Kuu ya chama hicho cha upinzani kumteua wakitaka mgombea wao, Hijja Ramadhan arudishwe jambo lililofanya Nkumba kuondolewa na kukosa nafasi ya kugombea ubunge.
Nkumba alipojitoa CCM alisema alikipenda kwa dhati chama hicho lakini hakuona sababu ya kuendelea kubaki kwa kuwa hasikilizwi na hakina mapenzi na watu.
Lakini akizungumza Dar es Salaam jana, Nkumba alisema amerudi nyumbani kwa kuwa alipotea njia na hakuona kama kuna mwelekeo Chadema.
Alipoulizwa kuhusu kupewa jimbo na Chadema alisema hayo yaachwe, amerudi nyumbani kwa kuwa ni kama rebound katika mchezo wa kikapu na watu wanaendelea kucheza.
Katibu wa CCM Wilaya ya Sikonge, Seleman Majilanga alisema hakuna tatizo kwa Nkumba kurejea ilimradi afuate taratibu.
. “Unajua ukishahama chama, kadi yako inakuwa haina kazi na inabidi uanze upya na yeye inabidi aende kwenye tawi lake,” alisema.
Majilanga alisema hana tatizo kumpokea mwanachama mpya au anayerudi na hajawahi kuzungumza na Nkumba kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ndani ya chama katika kura za maoni.
“Sisi tumejipanga kufanya kampeni zetu na kushinda bila yeye na kwa uhakika ushindi ni mkubwa katika jimbo letu,” alisema.
Post a Comment