Mwenyekiti wa Vijana Chadema Tawi la Luis, Mbezi Luis, Dar es Salaam, Dennis Kasanga ameuawa kwa kupigwa risasi shingoni usiku wa kuamkia jana, huku taarifa zilizotolewa na polisi zikitofautiana na mashuhuda wa tukio hilo.
Kasanga,
mkazi wa Mbezi Luis alipigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa majambazi
waliovamia baa inayojulikana kwa jina la Mtauli iliyopo njiapanda ya
Barabara ya Goba na Makabe saa saba usiku. Hata hivyo, polisi wamesema
tukio hilo halihusiani na ujambazi na wala halikutokea muda huo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alisema jana
kuwa tukio hilo lilitokea saa 10 alfajiri kuamkia jana.
Alisema
tukio hilo lilitokea Barabara ya Goba baada ya watu wanne waliokuwa
wakisukuma gari bovu kuvamiwa na watu wengine wanne na kuibuka mzozo
kati yao.
“Baada
ya mzozo, ghafla mmoja aliibuka na kuanza kuwafyatulia risasi
iliyowajeruhi watu wawili na kuua mmoja aliyepigwa risasi shingoni,” alisema Kamanda Wambura.
Kamanda Wambura alisema tukio
hilo halihusiani na ujambazi kama watu wanavyodai. “Siyo kila mtu
anayefyatua risasi ni jambazi, subiri kwanza tunaendelea na uchunguzi wa
tukio.”
Hata
hivyo, mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa marehemu aliuawa kwa
kupigwa risasi na majambazi, ambao pia waliwajeruhi watu wengine wawili
akiwamo mlinzi wa baa hiyo.
Mbali
na kujeruhi, watu waliokuwa na bastola, mapanga na marungu pia
waliwapora simu na fedha wateja wachache waliokuwapo kwenye baa hiyo.
Kati
ya waliojeruhiwa, mmoja ni mlinzi aliyepigwa rungu usoni na mwingine
aitwaye Erasmo Basheja, mkazi wa eneo la Basondole aliyepigwa risasi
begani.
Mhudumu
mmoja wa baa hiyo aliyekataa kutaja jina lake, alisema jana kuwa watu
kati ya sita au saba walifika kwenye baa hiyo saa saba usiku wakijifanya
wateja waliotaka kuhudumiwa vinywaji.
Alisema wakati wakifika, baa ilishafungwa ila kulikuwa na wateja wachache nje na yeye muda huo alikuwa ndani. “Baa ilishafungwa zamani, ila kulikuwa na wateja wachache nje wakimalizia vinywaji,” alisema shuhuda huyo.
Alisema
baada ya watu hao kuelezwa kuwa baa imeshafungwa, ghafla walibadilika
na kuwataka watu waliokuwa hapo kulala chini na wakaanza kuwapekua
mifukoni na kupora simu zao.
“Nilisikia
mlio wa risasi na haraka haraka nilifunga mlango wa kuingia kaunta ya
vinywaji kisha nikalala uvunguni kwenye chumba kinachotumia mlango mmoja
na kaunta,” alisema shuhuda huyo.
Aliongeza: “Niliwasikia wale majambazi wakisema, ‘hawa wanawake wameshafunga geti.’ Nilikaa kimya nikiwa nimejilaza chini ya godoro.”
Alisema
majambazi hao wanaijua fika baa hiyo, kwani baada ya kuwalaza watu
chini walizunguka nyuma, ambako ndiko kwenye geti la kuingia kaunta na
vyumba vya ndani.
Mlinzi
wa baa hiyo, ambaye amejeruhiwa usoni kwa kupigwa na rungu alisema kuwa
majambazi hao walifika kwenye baa hiyo saa saba usiku wakati tayari
pameshafungwa.
Alisema
alikuwa amekaa kaunta pamoja na marehemu na mtu mwingine ambaye
hakumbuki jina lake, ndipo aliposikia mlio wa risasi na wakati
akitaharuki, alivamiwa na mmoja wa watu hao na kupigwa rungu usoni huku
akisema: “Usiniangalie usoni.”
“Nilidondoka
chini na wakaanza kunisachi mifukoni huku wakinitaka kutoa simu na
fedha, niliwajibu sina kitu na baada ya kunipiga niliamua kutoa simu na
kuwapa,” alisema mlinzi huyo.
Alisema marehemu alipigwa risasi wakati akiondoka alipoketi na kwenda sehemu ambayo alisikia mlio wa risasi.
“Alikuwa kaunta na baada ya mlio wa risasi alinyanyuka na kwenda sehemu
ya nje ya baa huko ndiko alikopigwa risasi na kufariki dunia papo
hapo,” alisema.
Kifo cha kiongozi huyo wa vijana Chadema pia kimethibitishwa na mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Luis, Finna Massawe.
Post a Comment