0

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umeishauri  Serikali kuwachia askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kazi ya uhakiki na ugawaji wa misaada yote kwa waathirik
a wa janga hilo la tetemeko la ardhi kuepusha kazi hiyo kuingiliwa na matapeli wa kisiasa.

UVCCM imesema viongozi wa Chadema mkoa wa Kagera wamekuwa  wakilitumia janga la tetemeko hilo la ardhi kufanya ng'iliba na propaganda za kisiasa  na hivyo mewataka viongozi wa chama hicho kuacha mara moja kulitumia janga hilo vibaya.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa UUCCM Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Salum Kijuu alipomtembelea ofisini kwake. .

Shaka  alisema kitendo kinachofanywa na viongozi wa Chadema ni kituko na fedheha ya kisiasa kuona viongozi hao wakilitumia tetemeko hilo kujaribu  kujijenga kisiasa na kuwabagua wanananchi kwa itikadi za kisiasa kinyume na ubinadamu.

Alisema uhakiki na utoaji wa misaada katika awamu ya kwanza ulifanyika kwa kuongozwa na vitendo vya ubaguzi na upendeleo huku baadhi ya shehena za mizigo ya misaada na vifaa  vya ujenzi ikiandikwa maneno "ukawa pamoja ".

"Kumefanyika ubaguzi na siasa potofu zikiongozwa na viongozi wa Chadema, tunaishauri na kuitaka serikali ili kuwakwepa matapeli wa kisiasa na ubabaishaji huu kazi ya uhakiki, uratibu na ugawaji wa misaada wachiwe  wanajeshi wa JWTZ 'alisema Shaka

Shaka alimueleza mkuu wa mkoa Kagera kwamba haitapendeza na dunia itawashangaa watanzania kuwaona baadhi ya watu badala ya kushughulikia majanga na kujali utu  wao wakitafuta sifa za kisiasa.

Pia alimfahamisha mkuu wa mkoa kwamba katika uhakiki wapo watu wanaomiliki nyumba zaidi ya moja lakini majina yao yanapoonekana zaidi ya mara moja wamekuwa wakisumbuliwa bila sababu .

"Mkuu ipo haja tujue kuwa kuna wamiliki wa nyumba na wapangaji wote hawa katika janga hili ni waathirika wa tetemeko , mmoja ikiwa amepoteza nyumba , wengine wamepoteza ndugu, mali na vifaa vyao muhimu vya kuendeshea maisha "alisema Katibu huyo

Akijibu maelezo hayo mkuu wa mkoa Meja Jenerali Kijuu alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa itachukua juhudi za kuchunguza na ikithibitika kuwepo kwa madai hayo haitasita kumchukulia yeyote hatua za kisheria .

"Dai hili nitalivalia njuga, vyombo vyetu vikileta taarifa na uthibitisho nitamchukulia yeyote hatua za kisheria, kwanini watu washindwe kutenganisha vipindi vya siasa, wakati wa kazi au wa kukabili majanga na misiba "alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Ujumbe wa uvccm ukiongozwa na Kaimu Katibu  Mkuu Shaka ulikabidhi kwa mkuu wa mkoa msaada wa   mifuko mia moja  ya saruji na mahema 4   sambamaba na kushiriki zoezi la kuchangia damu lililofanyika uwanja wa uhuru maarufu Mayunga

UVCCM walifika kukagua madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo pamoja na kufika kuhani msiba wa Katibu wa UVCCM kata ya Amgembe Manispaa ya Bukoba Marehemu Jonas Bushoke.

Msafara huo ulijumuisha wajumbe wa Baraza kuu Taifa wajumbe wa Secretariet pamoja na viongozi wengine waandamizi wa UVCCM Taifa na Mkoa wa Kagera.


Post a Comment

 
Top