0

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema leo amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, hadi kufikia Jumanne wiki ijayo, iwapo Jeshi la Polisi halitawape
leka mahakamani mahabusu wanaoshikiliwa katika vituo vya polisi kwa sababu za kisiasa litapeleka mashitaka Mahakama Kuu.
“Nimefanya mahojiano na watu 10 wanaoshikiliwa na kituo cha polisi cha Oysterbay na Kituo Kikuu cha Polisi cha kati. Mahabusu wa Oysterbay wamezungumza mbele ya mkuu wa kituo hicho kwamba wameteswa sana. Wakiwa chini ya ulinzi wa polisi wamepigwa sana.
“Huwa wanachukuliwa kutoka mahabusu usiku na kupelekwa mikocheni kwenye kituo cha mateso. Wanavuliwa nguo na wanapigwa hadi kuvuja damu. Wanawekwa katika vituo vya polisi zaidi ya wiki mbili bila kupelekwa mahakamani kwa sababu tu ya tuhuma,” amesema Lissu.
Lissu amewataja watu wanaoshikiliwa katika kituo cha polisi Oysterbay kuwa ni; Anstotle Mgasi na Hosia Mbuba waliokamatawa Vwawa, Juma Salum na Suleiman Said waliokamatwa Pemba, Dk. David Nikas aliyekamatwa Tunduma, Mdude Nyangali aliekamatwa Songea.
Wengine ni Shakira Makame na Ignas Mzenga. Baadhi ya mahabusu hao walikamatwa mikoani na kusafirishwa mpaka Dar, huku Ben Nzogu na Musa Sikabwe wakiwa wamehifadhiwa kituo cha kati (Central).
“Kwa kuwa Jeshi la Polisi, linakiuka katiba na sheria, ikifika Jumanne wiki ijayo halijawapeleka mahakamani watu hawa. Tutaenda Mahakama Kuu kwa kutumia utaratibu wa ‘Habeas Corpus’ ili jeshi hilo litaitwa na mahakama kueleza kwa nini linawashikilia watu hao kinyume na sheria,” amesema Lissu.
Amesema Chama hicho kina taarifa zisizo rasmi kwamba mpaka sasa nchi nzima wanashikiliwa jumla ya watu 73 kwa kile kilichoitwa, “kukosoa utawala wa Rais John Magufuli” ikiwemo kusambaza video inayomwenyesha Lissu akisema Rais Magufuli ni ‘dikteta uchwara’
“Mahakama lazima iwahoji polisi, kwa nini wanawashikilia na kuwatesa watu bila kuwapeleka mahakamani? Tusipowazungumzia hawa wasio viongozi basi watanzania wengi wataumizwa,” amesema Lissu.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, Jeshi la Polisi linatakiwa kumshikilia mtu kama mahabusu kwa muda usiozidi masaa 24 na baada ya hapo linatakiwa kumfikisha mahakamani.
Kifungu cha 360 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinaruhusu Mahakama Kuu, kutoa amri mtu yeyote ambaye anashikiliwa kinyume cha sheria kupelekwa mahakamani au kuachiliwa huru.


Post a Comment

 
Top