0
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.George Simbachawene ameuvunja mkataba baina ya mwekezaji wa kigeni na Kijiji cha Chole wilayani Mafia kwani Kijiji hakikuwa na haki ya kumiliki mali kale kwa sababu mali kale zote zinamilikiwa na Serikali kuu.

Mkataba uliovunjwa na Waziri Simbachawene ulikuwa ukiihusu Kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development Company LTD inayomilikiwa na bwana Jean Devillies na mkewe Ann Devillies na Kijiji cha Chole.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chole kilichopo katika kata ya Jibondo wilayani Mafia, Mheshimiwa Simbachawene alisema kuwa eneo la Mali kale ambalo zamani lilikaliwa na waarabu na baadaye wajerumani ni mali ya serikali kuu na kwamba Kijiji hakikuwa na nguvu ya kisheria ya kumiliki eneo hilo.
Waziri Simbachawene aliongeza kuwa mara baada ya nchi kupata uhuru mali kale zote zilichukuliwa na serikali kuu na kwamba kijiji bila kushirikisha serikali kuu kilikosa nguvu ya kisheria kumiliki eneo hilo.
"Mkataba huu ambao mwekezaji anaona ni mkataba sahihi kwake na unamfanya kuhisi kuwa ana haki zote, unaonekana una tatizo kwa sababu mkataba umeingiwa mwaka 2007 lakini kabla ya mwaka 2007 mwekezaji huyu alikuwa na hati," alisema.
Mheshimiwa Simbachawene alisema katika kipengele cha 227 kinaeleza kuwa ni kuiwezesha kampuni kupata hati miliki ya eneo kutoka kwa serikali ya Tanzania kwa ajili ya eneo lote ambalo kwa wakati huo lilikuwa tayari linamilikiwa na kampuni hiyo.
Waziri Simbachawene alifafanua kuwa kipengele hicho kina matatizo kwani maana yake ni kuwa kijiji kinatakiwa kiiwezeshe kampuni kupata hati wakati mkataba huo unaandaliwa tayari kampuni hiyo ilikuwa na hati.
Kipengele kingine kilichokuwa na utata kwa mujibu wa mkataba huo ni kile cha 228 ambacho kinasema kutoruhusu mtu yeyote au kampuni au taasisi yoyote bila makubaliano na kampuni isipokuwa kwa mkazi wa chole.
Waziri Simbachawene alisema kuwa kipengele hicho kinakiuka sheria za nchi kwa kuzuia wawekezaji wengine kufanya biashara ya utalii katika kijiji hicho.
Hivyo, Waziri alisema kuwa Kijiji hakikuwa na mamlaka ya kuingia mkataba na mwekezaji kwa ajili ya eneo la mali kale na hivyo mkataba huo ni batili na hauwezi kutambulika kisheria kama mwekezaji huyo anavyoamini.
Waziri Simbachawene alisema kuwa mkataba huo hauna nguvu ya kisheria na hivyo haupo, na kwamba mwekezaji huyo kwa sasa hana mamlaka ya kumiliki eneo hilo ambalo ni mali ya serikali kuu.

Post a Comment

 
Top