0
Mamlaka  ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali itakuwa na uwezo na mamlaka ya kuchunguza watu waliozaliwa na jinsi mbili na kubaini jinsi tawala yenye nguvu zaidi. 

Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016, uliopitishwa juzi usiku saa nne bungeni unampa Mkemia Mkuu mamlaka ya kuchunguza na kubaini jinsi ya mtu na kutatua utata kwa mtu atakayekuwa amezaliwa na jinsi mbili.

“Waheshimiwa wabunge naona wengi wenu mnadhani mkemia mkuu kazi yake ni kuchunguza vinasaba kubaini uhalali wa mzazi na mtoto, maana naona wabunge wengi wamelishabikia hilo, lakini katika teknolojia ya vinasaba yanahusu pia utambuzi wa jinsi, watu unakuta wanawake au wanaume wanazaliwa jinsi ya kike na kiume, kwa hiyo tunaangalia jinsi tawala ni ipi ina nguvu,” alisema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Ummy alikuwa akijibu michango ya wabunge waliochangia wakati wa kujadili Muswada wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 kabla ya kuupitisha juzi usiku, waliotaka mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu kutoa elimu kwa wananchi juu ya shughuli zake.

Alisema kwa sheria hiyo, sasa mkemia mkuu kupitia maabara yake anaweza kusema jinsi ya kike au ya kiume ndio yenye nguvu, lakini pia kuna suala la kuhakikisha utambuzi wa mwanadamu hasa wakati yanapotokea majanga pamoja na watu wanaosafiri kwa makundi.

Alikubaliana na wabunge kuwa iko haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya kazi za maabara ya mkemia mkuu ambao wengi wao wanadhani inafanya kazi hiyo tu ya kubaini vinasaba vya mzazi na mtoto, lakini sasa wafahamu hata waliozaliwa na jinsi mbili wanaweza kutegua utata huo kwa kubaini jinsi tawala au jinsi yenye nguvu zaidi kama ni ya kiume au ya kike.

Alisema Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwepo kihistoria tangu mwaka 1890 na imekuwa chombo cha kiserikali cha uchunguzi cha kikemia wa kimaabara kwa bidhaa mbalimbali na kuongeza kuwa imekuwa ikifanya uchunguzi wa kikemia wa vyakula, dawa na vipodozi hasa pale inapotokea utata au kuhusisha masuala ya kesi za jinai.

Akifafanua zaidi, alisema kwa upande wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wao wanafanya udhibiti wa ubora wa chakula, dawa na vipodozi na maabara hii inafanya uchunguzi wa kikemia.

“Maabara ya Mkemia Mkuu kazi yake ni kufanya uchunguzi wa kikemia, vinasaba, kesi za jinai na sayansi jinai. Chombo hiki hakipimi kudhibiti ila kufanya uchunguzi kwa ajili ya vitu vyenye maslahi ya taifa au masuala yenye utatanishi na ushindanishi,” alisema waziri huyo.

Akitoa mfano wa mahindi, alisema kulikuwa na tatizo la sumu kuvu, kwa hiyo mkemia mkuu anafanya uchunguzi wa kimaabara na kusema wamekuta mahindi yana sumu au la, au anaweza mfanyabiashara kuleta maziwa ya mtoto TFDA ikapata mashaka, mkemia mkuu atayafanya uchunguzi wa maabara atasema kama kuna sumu ama kuna kemikali isiyo salama kwa matumizi wa binadamu.

“Baada ya uchunguzi wa kimaabara mwenye jukumu la kusema mahindi haya yasiuzwe au maziwa haya yasiuzwe ni TFDA na sio maabara ya mkemia mkuu. Vile mfanyabiashara anaweza kuleta bidhaa, TFDA ikaitilia mashaka, kwa hiyo huyu mwenye bidhaa anaweza kukata rufaa kwa mkemia mkuu ili apimiwe bidhaa yake kuithibitishia TFDA kuwa bidhaa yake ni salama,” alisema.

Waziri Ummy alikuwa akijibu hoja za wabunge, ambao walikuwa wana hofu kuwa Maabara ya Mkemia Mkuu inaweza kuingilia kazi za taasisi kama TFDA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Alizungumzia pia kuhusu kuipa mamlaka ya mwisho maabara hiyo, akisema katika nchi zote duniani zenye maabara hizo, lazima serikali iwe na msemaji wa mwisho wa uchunguzi wa masuala ya kimaabara na kikemia, vinasaba, sayansi jinai na kesi za jinai, lakini pia haifuti sheria wala maabara zingine za uchunguzi zilizoanzishwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali.

Kuhusu kutenga bajeti ya kutosha, Ummy alisema serikali imepokea maoni ya wabunge na kuwa baada ya kupitisha muswada huo maabara hiyo imepewa hadhi ya mamlaka na sasa imepewa hadhi na hivyo fungu lake lazima liwe zuri kwa ajili kuendesha shughuli za maabara lakini pia kuajiri watumishi 400 kwani waliopo sasa 192 hawatoshi.

Waziri Ummy alisema wamepokea ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, kufanya uchunguzi wa matumizi ya shisha na kuongeza kuwa tayari mkemia mkuu alifanya uchunguzi na kubaini watumiaji wa shisha wanachanganya bangi, heroine na kokeni na ndio maana serikali ilipiga marufuku kuitumia.

Hata hivyo, alisema sasa itajikita zaidi kuchunguza ili kubaini viambata kiasi gani vilivyopo katika shisha na kwa nini serikali iendelee kupiga marufuku matumizi ya shisha nchini.
 
Hii inamaana kwamba kama wakibainika wapo wataruhusiwa kufanya ivyo.

Post a Comment

 
Top