Mahakama Kuu imezuia kupigwa
mnada kwa vifaa vya kampuni ya Mbowe Hotels, inayomilikiwa na mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe kutokana na mzozo wa kodi ya pango baina ya kampuni hiyo
na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji
Sivangilwa Mwangesi wakati akisikiliza maombi ya Mbowe Hotels Ltd dhidi ya
NHC na kampuni ya udala
li ya Fosters Auctioneers and General Traders.
Fosters ndiyo
iliyopewa na NHC kazi ya kuondoa vifaa vya kampuni ya mbunge huyo wa Hai kutoka
kwenye majengo yaliyoko Mtaa wa Mkwepu, ambako kulikuwa na klabu maarufu ya
usiku ya Bilicanas na ofisi za Free Media, zote zikimilikiwa na mwanasiasa
huyo.
NHC inadai kuwa Mbowe
ameshindwa kulipa kodi ya pango ya Sh1.2 bilioni, jambo ambalo mwenyekiti huyo
wa Chadema analipinga.
Katika maombi hayo, Mbowe
anaiomba Mahakama iiamuru NHC na Fosters kumrejesha kwenye jengo hilo pamoja na
mali na vifaa vyote vilivyochukuliwa na kampuni hiyo ya udalali.
Maombi hayo ya Mbowe
yalikuwa yasikilizwe, lakini NHC waliweka pingamizi la awali wakiiomba mahakama
iyatupilie mbali wakidai kuwa ni batili kwa kuwa yamefunguliwa chini ya kifungu
cha sheria kisicho sahihi.
Kufuatia maombi hayo,
mawakili wa Mbowe, wakiongozwa na Peter Kibatala, waliomba pingamizi hilo
lisikilizwe kwa pamoja na maombi hayo.
Kibatala amesema maombi ni
halali na kwamba kifungu cha sheria walichotumia ni sahihi kulingana na
mazingira ya mgogoro huo.
Hata hivyo, mahakama iliamua
kusikiliza pingamizi hilo kwanza.
Baada ya uamuzi huo,
Kibatala aliomba mahakama itoe amri ya zuio la muda ili NHC isitekeleze azma
yake ya kuzipiga mnada mali na vifaa hivyo.
Post a Comment