TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waheshimiwa wanahabari,
Awali napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa kuitikia wito wetu, nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kutupasha habari mbalimbali zinazohusiana na hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya nchi yetu na nje ya mipaka yake.
Lakini pia kuwapa pole kutokana na namna mnavyotekeleza majukumu yenu katika mazingira magumu ya hofu na vitisho vinavyofanywa na watendaji wa serikali ya awamu ya tano.
Nitumie fursa hii pia kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza rasmi kuzungumza na vyombo vya habari toka BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA liniamini na kunipa dhamana kubwa ya utendaji na usimamizi wa chama chetu kwa kuniteua kuwa MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI WA CHAMA CHETU CHA WANANCHI CUF TAIFA, tukisimamia majukumu yaliyopaswa kufanywa na Mwenyekiti wa Chama Taifa na Makamu Mwenyekiti Taifa.
Naahidi nitatekeleza wajibu wangu kwa uaminifu mkubwa na weledi wa hali ya juu kwa madhumuni ya kuwaletea watanzania mabadiliko sahihi ya maendeleo ya kisiasa na kiuchumi wanayoyataka katika Taifa letu.
Waheshimiwa wanahabari,
Tumewaiteni na kuomba kuzungumza nanyi kwa lengo la kujibu kauli zilizotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alizozitoa juzi na jana (tarehe 2-3/9/2016) katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika kisiwa cha Pemba, uwanja wa Gombani na Unguja katika uwanja demokrasia (Kibandamaiti) na kupitia nyinyi tufikishe ujumbe wetu kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais JOHN MAGUFULI na watanzania kwa ujumla. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amezungumza mambo mengi na pia amejikita katika kutoa kauli za dhihaka na mipasho dhidi ya Chama cha Wananchi CUF na katibu mkuu wetu Maalim Seif Sharif Hamad jambo ambalo tunaamini kwa hadhi na heshima ya nafasi yake na hadhi ya taasisi ya urais hakupaswa kufanya hivyo kama kiongozi wa nchi.
Pamoja na masuala mengine Mwenyekiti wa CCM, Rais JOHN MAGUFULI amesema amekwenda kuwashukuru wananchi wa Unguja na Pemba kwa kumchagua yeye pamoja na Dokta Ali Mohamed Shein, amewahahakishia Wazanzibari kuwa atailinda amani ya nchi kwa nguvu zake zote na yeyote atakayejaribu kuivuruga amani atamshughulikia kwa nguvu zake zote bila huruma, ataulinda Muungano kwa nguvu zake zote na lazima uendelee kudumu katika kipindi chote cha utawala wake.
Tatu, amezungumzia maendeleo – Maji, viwanda, miundombinu, uvuvi na kadhalika lakini pia amezungumzia kuitunza amani akitolea mifano ya nchi zisizokuwa na amani ikiwemo Libya, Iraq, Syria, Somalia na mauaji ya kimbali yaliyotokea Rwanda mwaka 1994.
Magufuli amepongeza aliyooiita “kazi nzuri ya majeshi” nadhani kwa kuisaidia kupata ushindi na kuwathibiti wanaotaka mabadiliko na amempongeza Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC, kwa kufuta uchaguzi wa tarehe 25/10/2016 uliompa ushindi Maalim Seif Sharif Hamad, na kumuombea apewe tuzo kwa kazi nzuri aliyoifanya.
Anashangaa kwanini Dokta Shein ameunda serikali kwa kuvishirikisha vyama vingine wakati alishinda (Shein) kwa asilimia 99 huku akijigamba kuwa yeye kamwe hawezi kuingiza na hataingiza mtu hata mmoja kutoka upinzani katika serikali yake pamoja na kupata ushindi wa asilimia 58 anasahau kuwa hivi karibuni amemteua Mwenyekiti wa TLP Mhe. Agustino Lyatonga Mrema, kuwa Mwenyekiti wa bodi ya PAROLE.
MSIMAMO WA CUF JUU YA KAULI ALIZOZITOA RAIS MAGUFULI:
1. THE CIVIC UNITED FRONT (CUF CHAMA CHA WANANCHI) kimesikitishwa na kauli zisizofaa kwa heshima na hadhi ya taasisi ya urais na nafasi yake kama kiongozi wa nchi kutoka kauli za uchochezi, kupandikiza chuki na uhasama, kuwagawa wananchi na kutaka kujenga chama chake kwa njia ya vitisho na kutumia vyombo vya dola.
Tunamtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli atambue kuwa hatoweza kujenga umoja wa watanzania kwa kutoa kauli za kuimarisha chuki, uhasama na kutosimamia haki, na kuunga mkono vitendo vya uvunjaji wa demokrasia na sheria za nchi.
Rais Magufuli hawezi kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi vijavyo katika mikakati ya mataifa masikini ya kulinda sheria, haki za kiraia, utawala bora na kuleta maendeleo shirikishi (Inclusive Develeopment).
2. Kauli nyingi za kuchochea chuki na uhasama alizozitoa Rais Magufuli si za kwanza wala si ngeni kwa Wazanzibari. Kisiasa wazanzibar na hasa wafuasi wa CUF (ambao ni wengi) wamekuwa waathirika wakubwa wa matumizi makubwa ya ukandamizaji na unyanyasaji iunaofanywa kikatili sana kupitia MAJESHI, MAZOMBI, JANJAWIDI nakadhalika.
Mauaji yaliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya utawala wa serikali ya awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamini William Mkapa Januari 26-27, 2001 yalisababisha watu 46 kuuliwa na vyombo vya Ulinzi, watu 38 wameuwawa kwa kificho mpaka leo hawajaonekana. Watanzania 658 waliojeruhiwa, na 135 waliopata vilema vya kudumu katika maisha yao.
Aidha zaidi ya wazanzibar 4000 waliishi kama wakimbizi Shimoni, Mombasa nchini Kenya, orodha yao tumeiambatanisha na taarifa hii. Kama kweli Rais Magufuli anataka kulinda amani ya Tanzania haiwezekani kuwa raia wamekuwa wakipigwa na kuteswa na kukatwa viungo vyao na kuporwa mali zao na vikosi vya majeshi, Mazombi na akiwa kimya na kutoa kauli za kubariki vitendo hivyo.
Kwa mtizamo wa Magufuli, ukatili na uhuni unaotendwa na MAZOMBI ukiungwa mkono na vikosi vya majeshi ya SMZ na vile vya Muungano eti ndiyo ulinzi wa amani. Lakini, Kauli mfano wa hizi zimewahi kutolewa na watangulizi wake na viongozi wa Zanzibar waliopita.
Hata hivyo mwisho wa yote hawakuweza kufanikiwa kuwahadaa wazanzibari kudai haki yao na mwaka hadi mwaka wazanzibar wanaotaka mabadiliko wawekuwa wakiongezeka na kuidhihirishia dunia kuwa hawawezi kuvunjwa moyo na vitisho, hujuma na ukandamizaji.
3. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amemsifia Dokta Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wazanzibar kwa kura nyingi. Jambo hili linachekesha na kustaajabisha dunia, kwani Hata mtoto mdogo anayeishi Zanzibar au Tanganyika anatambua kuwa Dr. Shein si rais halali wa Zanzibar.
Ni rais aliyeingizwa madarakani kwa kile kinachoweza kuitwa “tyranny of the highest order of the African Power Mongers who are ready to shed blood for power” yaani “udhalimu wa kiwango cha juu kabisa kinachofanywa na viongozi waroho wa madaraka ambao wako tayari kumwaga damu ili watawale”.
Katika uchaguzi halali wa tarehe 25/10/2016. Wazanzibar walimchagua kwa kura nyingi kabisa, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wao. Wazanzibari wanajua hivyo, Watanzania wanajua hivyo, Waafrika wanajua hivyo na dunia inaimba wimbo huo. Kujidanganya kuwa Dokta Shein ni rais halali wa Zanzibar ni uotaji wa ndoto ya mchana kuwa Tanzania ina viwanda kila kata na kila kijiji, ndoto ambayo kwa aina ya uongozi wa John Magufuli haiwezi kutimia.
TAKWIMU ZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA TAREHE 25/10/2015:
Wapiga kura wote wa NEC Zanzibar ni 417,882. Kura alizopata LOWASSA 211,033 = 50.05% kura alizopata MAGUFULI ni 194,317= 46.50% Ushindi wa kura za lowassa dhidi ya Makufuli ni 16,721.
ZEC wapiga kura wote ni 402,354. Kura alipigiwa Maalim Seif ni 207,847 =53.32%. kura alizopata Dokta Ali Mohamed Sheni ni 182,011 =46.68%. Ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad dhidi ya Dk Sheni ni kura 25,836.
Kwa matokea haya ni wazi kuwa Wanzanzibar wameikataa CCM. Wazanzibar hawakuwachagua wagombea wa CCM John Magufuli na DK Shein wake.
4. THE CIVIC UNITED FRONT (CUF CHAMA CHA WANANCHI) kinaendelea na msimamo wake uliotolewa na kikao cha Baraza KUU la uongozi Taifa kilichofanyika tarehe 2-3 April, 2016 wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao.
CUF itaendeleza msimamo wake wa kutoshirikiana na Serikali haramu iliyoundwa na dokta Shein kutokana na uchaguzi batili uliofanyika kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi.
Kwa vyovyote vile, Serikali ya dokta Shein haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ya nchi.
5. Chama Cha Wananchi CUF, kinaendelea na msimamo wake wa kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na uliofanyika katika hali ya amani na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo yake ambayo yanaonyesha wazi kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif Sharif Hamad Kitendo cha zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari kususia uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa nguvu maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Chama cha CUF na Viongozi wake hawawezi kuyumbishwa na watu wenye weledi mdogo sana na siasa za Zanzibar, kama alivyoonesha Rais John Pombe Magufuli. Vitisho vyote vilivyotolewa na Magufuli dhidi ya wanaosimamia HAKI SAWA KWA WOTE na misingi ya kidemokrasia, havitarudisha nyuma juhudi za kuijenga Zanzibari na Tanzania mpya.
6. Tunamtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli afahamu kuwa stahiki zote anazopewa Maalim Seif zipo kisheria kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama wanavyopewa viongozi wastaafu wengine hapa nchini.
Stahiki hizo si hisani inayotoka mfukoni mwa kiongozi yeyote Yule. Wala si fedha za CCM, ni fedha za watanzania zinazotokana na makusanyo ya kodi zinazolipwa na wananchi.
Sheria ya Mafao ya Viongozi wastaafu wa Kisiasa ya Zanzibar (The Political Leaders Retirement Benefits Act) namba 6 ya mwaka 1999 iliyopitishwa na Dr. Salmin Amour tarehe 15 Mei 2000) imeeleza wazi kuwa viongozi wote wa kisiasa waliohudumu katika serikali ya Zanzibar kuanzia mwaka 1995 kwenda mbele watakuwa na haki isiyoondolewa kwa namna yoyote, ya kupokea stahiki zote muhimu kama viongozi wastaafu.
Rais Magufuli amekuwa rais wa kwanza Tanzania mwenye kutoa kauli zenye ukakasi kwa jamii, zenye kugongana na tabia ya kufanya maamuzi bila kuangalia katiba na sheria za nchi. kwake yeye urais siyo taasisi, ni mtu, kwa Magufuli urais ni ubabe, dhuluma, vitisho, kukandamiza na kutojali katiba na sheria za nchi.
Huenda Taifa letu limepata janga kubwa la kitaifa katika awamu hii ya uongozi wa nchi. Ni jambo la aibu sana kuona rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavunja sheria za nchi yake na anamhamasisha rais wa Zanzibar afanye kama anavyofanya yeye.
7. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli anazungumzia kulinda amani bila kuzungumzia kulinda haki. Na wakati huo huo anachochea matumizi makubwa ya kijeshi yasiyozingatia sheria kwa wananchi. Mifano aliyoitoa ya nchi zilizoingia katika uvunjifu wa amani haina uhusiano kabisa na masuala yanayoendelea katika nchi yetu.
Rais Magufuli anasahau kuwa nchi hizo anazozitolea mifano, ziliharibiwa kwa sababu ya kuwa na viongozi walioamini katika nguvu za kijeshi (kama yeye) kuliko uongozi wa kidemokrasia na wa kufuata sheria. Raia wa nchi hizo anazozitaja Magufuli walinyimwa haki za msingi za muda mrefu na watawala ndipo wananchi walipoanzisha harakati za kujikomboa, majeshi yaliyoziunga mkono hayakuweza kuzima nguvu ya mabadiliko.
Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kuwa na rais ambaye kila kukicha mahubiri yake ni namna gani “majeshi yake yatawashughulikia raia wa nchi yake”.
Hizi ni hotuba zinazowafanya wananchi wajiandae kisaikolojia kupambana na majeshi yao. Watanzania hawakumchagua Magufuli ili ayaandae majeshi kwa ajili hiyo, alikabidhiwa nchi hii ikiwa na amani na CUF haitakuwa tayari kumuona anaiingiza katika migawanyiko, vitisho na visasi ambavyo vinaweza kuzaa machafuko.
8. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar –ZEC (Jecha SALIM Jecha) kuhudhuria na kushiriki katika mkutano wa CCM uliofanyika Unguja ni ushahidi tosha kuwa tume ya uchaguzi ya ZEC si chombo kilicho huru na kwamba tume hiyo ipo hapo kuhakikisha kuwa Serikali ya CCM haiondolewi madarakani na wananchi wanaotaka mabadiliko ya uongozi wa kisiasa nchini na kwamba ZEC ni tawi la CCM linalotekeleza matakwa yao.
Kwa msingi huo huo, CUF na vyama vingine ambavyo vinapigania mabadiliko hapa Tanzania vitaendeleza mipango imara ya kupigania kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar na Tanzania Bara (NEC na ZEC).
Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kujisifia ushindi wa kupora katika uchaguzi kutokana na kupendelewa na Tume ya Uchaguzi ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
9. Tunamtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli atambue kuwa; CUF ni taasisi kubwa ya kisiasa nchini iliyo na wawakilishi wa kuchaguliwa na wananchi kutoka kila kona ya nchi yetu, CUF ina wabunge 18 kutoka Pemba, inawabunge wanne (4) kutoka unguja, inawabunge 10 kutoka Tanzania bara.
CUF ni chama cha kitaifa kweli, na tangu mwaka 1995 mpaka sasa CCM haijawahi kupata kiti hata kimoja cha uwakilishi toka Pemba. Magufuli asaidiwe na chama chake, kwamba matamanio yake ya kuifanya Tanzania iwe nchi ya mapambano ya kijeshi na raia hayatafikiwa.
Akumbushwe kuwa kauli zake zimejaa uchochezi wa kila namna anajaribu kuwaghadhibisha wananchi (Provoke), ghilba za kisiasa za waziwazi na nia ovu iliyojaa visasi. Kauli za namna hii akiendelea kuzitoa katika kipindi cha miaka yake mitano, ataimaliza huku kila mtanzania akijiridhisha kuwa nchi ilipata rais ambaye hakujua nini maana ya urais, na kwa vyovyote vile hakuwatendea haki waliomchagua.
Mwisho:
Sote tunatambua kuwa Serikali ya CCM kwa kumtumia Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli imeshindwa katika ulingo wa kisiasa kwa kushindana kwa hoja, imekosa uvumilivu wa kisiasa na badala yake inaendesha nchi kwa mfumo wa mabavu bila kuzingatia sheria, haki na wajibu, taratibu na kanuni. Hebu tujiulize, ni nchi gani duniani ambayo ilishinda NGUVU YA UMMA INAYOTAKA MABADILIKO?
Madhumuni ya harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu miaka ya 1953-1961 yalikuwa na lengo la kutuondoa watanganyika kutoka katika utumwa, unyonyaji, unyanyasaji, ukandamizaji, ubepari na ubeberu wa rasilimali za Taifa letu na watu wake. Jeshi la mkoloni lilikuwa likitumika kuwadhalilisha wazee wetu.
Leo hii baada ya miaka 55 ya kujitawala, tukiwa ndani ya mfumo halali wa kisheria wa demokrasia ya vyama vingi nchini, serikali ya CCM kwa kumtumia Rais John Magufuli inaturudisha nyuma na kufanya vitendo vibaya zaidi kwa raia wake kuliko ilivyokuwa ikifanywa na wakoloni! Cha kusikitisha takwimu hazionyeshi jeshi la polisi lilipotumia nguvu kubwa kupambana na raia kisha raia wakafungua mashtaka mahakamani, Serikali (Jeshi la polisi) ni lini lilishinda kesi hizo. Mauaji ya mwandishi David Mwangosi ni ushahidi wa hili na kesi nyingine nyingi orodha ni ndefu ambazo zikifikishwa mahakamani haki inaangukia kwa walioshtakiwa?
Tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa kamwe hatoweza kuzuia nguvu kubwa ya watanzania iliyo tayari kuleta HAKI SAWA KWA WOTE na mabadiliko sahihi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kuboresha hali za maisha na kipato cha mtanzania kwa kutumia vyema rasilimali za nchi yetu. Tuna kila sababu ya kuunganisha nguvu zetu kama watanzania kumzuia Rais kwa njia ya amani asiendelee kuikanyaga katiba ya nchi aliyoapa kuilinda.
Tunahitaji Taifa letu liwe salama na hatuhitaji kwa namna yeyote ile uvunjwaji wa sheria na matumizi ya nguvu kubwa za vyombo vya dola yanayoandaliwa na rais mwenyewe ili yafanywe dhidi ya wananchi wadai demokrasia.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi) Kinawataka watanzania wote bila ya kujali itikadi za vyama vyetu kusimama imara kutetea misingi ya uongozi wa Taifa letu kwa kuilinda na kuihifadhi katiba na sheria za nchi yetu na kuhakikisha zinaheshimiwa, zinafuatwa na kuhifadhiwa na kila mmoja wetu.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) tunawahakikishia watanzania wote kuwa daima tutaendelea kusimama imara na kuwaunganisha watanzania wote ili kuimarisha umoja na mashirikiano baina yetu ya KUDAI HAKI SAWA KWA WOTE NA DEMOKRASIA YA KWELI kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
HAKI SAWA KWA WOTE
___________________________
JULIUS MTATIRO
MWENYEKITI KAMATI YA UONGOZI CUF -TAIFA
juliusmtatiro@yahoo.com
Mawasiliano:
Salim Bimani - 0777414112
Mkurugenzi habari, uenezi na mahusiano na ummah
Mbarala Maharagande
Naibu Mkurugenzi
Post a Comment