Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambavyo ni Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa Mazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani na kampuni ya
Peoples’ Media Communication Limited (PMCL) inayoendesha kituo cha Uhuru Fm, imejiuzulu leo.Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, imesema, Bodi hiyo iliyodumu kwa mihula miwili, imetangaza kujizulu kupitia barua ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo Al-haj Adam Omar Kimbisa. Wajumbe wa Bodi hiyo ni Katibu Gabriel Athumani ambaye alichukua nafasi hiyo hivi karibu baada ya kuachwa wazi na Katibu wa kwanza wa Bodi hiyo Daniel Godfrey Chongolo ambaye alijizulu.
Baadhi ya waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo ni Jack Gotham, Tatu Abdallah, Yusuf Chunda, Peter Machunde, Nora Mkami na Balozi Liundi.
"Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli amepokea barua ya kujiuzulu kwa bodi hiyo Septemba 22, 2016, ambayo nakala yake imenakiliwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana na barua hiyo inaeleza kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa Bodi hiyo wameamua kwa hiyari yao kujiuzulu nafasi zao", imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Hatua hiyo ya kujiuzulu, imekuja siku tatu, baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli kufanya ziara ya kustukiza kwenye Ofisi za Uhuru Publications Limited, Wachapishaji wa Magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, na kuzungumza na wafanyakazi.
Katika mazungumzo wafanyakazi walimpatia malalamiko mengi ikiwemo kuuzwa mtambo uliokuwa wa kuchapisha magazeti uliokuwa unamilikiwa na UPL chini ya kampuni tanzu ya Mordern Newspaper Printer (MNP) ambapo wafanyakazi walidai mtambo huo umeuzwa kama chuma chakavu na katika mazingira ya kutatanisha.
Katika baadhi ya malalamiko, wafanyakazi hao walimwambia pia Rais Dk. Magufuli kwamba walikuwa hawajalipwa mishahara kwa miezi saba sasa, na hali kadhalika mafao yao yalikuwa hayajapelekwa kwenye Mfuko wa NSSF tangu mwaka 2011.
Baadaye Dk. Magufuli alionyesha kustushwa na hali hiyo na kuonyesha kutaka kuivunja bodi lakini Katibu Mkuu wa CCM, Abdu;rahman Kinana akamweleza kuwa ili kuvunjwa Bodi hiyo ni lazima kwa mujibu wa utaratibu Kamati Kuu ya CCM iketi na kuridhia.
Bodi hiyo ya Uhuru Media Group ndiyo iliyokuwa na majukumu ya kusimamia, kuzielekeza na kuzishauri Menejimenti za Kampuni hizo za UPL na PMCL na kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vyombo hivyo vya habari vya Chama.
Post a Comment