Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa
madini kwenda kuuchenjua nje ya nchi akitaka shughuli hizo zifanyike
nchini, imeelezwa kuwa utekelezaji wa dhamira hiyo utachukua muda mrefu
kutokana na mchakato wake.
Juzi, Rais Magufuli alinukuliwa na
vyombo vya habari wilayani Kahama akisema katika uongozi wake hataki
kuona mchanga huo ukisafirishwa.
Alisema katika nchi zote zenye
madini, Tanzania ndiyo pekee inayosafirisha mchanga kwenda nje hivyo
akaagiza shughuli hiyo ifanyike nchini.
Agizo hilo limekuja
wakati utafiti juu ya uwezekano wa Tanzania kuwekeza katika mtambo wa
kuchenjua mchanga wa dhahabu ya uliofanywa na Wakala wa Ukaguzi Madini
Tanzania (TMAA) Februari 2011, ukionyesha kuwa ni uwekezaji unaohitaji
fedha nyingi.
Ripoti hiyo ilisema gharama za usimikaji mtambo kamili
wenye uwezo wa kuchenjua wastani wa tani 150,000 kwa mwaka, ingeweza
kufikia Dola za Marekani 500 milioni hadi Dola 800 milioni (sawa na
Sh1.1 trilioni hadi Sh1.74 trilioni za sasa).
Ripoti hiyo ambayo
ilikuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa kuchenjua mchanga
unaosafirishwa na kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya dhahabu ya
Buzwagi na Bulyanhulu, ilieleza kuwa baadhi ya mataifa yanayosafirisha
mchanga huo kwenda Japani na China ni Chile, Indonesia, Peru, Marekani,
Australia na Canada.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgodi wa Barrick
(sasa Accacia) huzalisha na kusafirisha kati ya tani 25,000 na 50,000
za mchanga huo kwa mwaka ili kuchuja kiwango cha madini yaliyomo.
Akitoa
maoni yake binafsi kuhusu agizo hilo, Makamu wa Rais wa Acacia, Deo
Mwanyika alisema msimamo wa Rais Magufuli ni sahihi lakini utekelezaji
wake utahitaji maandalizi kutokana na ukubwa wa gharama za uwekezaji wa
mtambo huo.
Huku akisisitiza kuwa maoni hayo ni yake binafsi,
Mwanyika alisema ipo haja ya Serikali na sekta binafsi kukaa pamoja kwa
ajili ya kujadili shughuli za uwekezaji huo hapa nchini.
“Nimemsikiliza
Rais na nimemwelewa dhamira yake lakini hajamaanisha amezuia rasmi,
haiwezekani kuzuia ghafla shughuli hizo. Pia sisi (wazalishaji) ni
tofauti kabisa na sekta hiyo ya uchenjuaji, kwa hiyo itabidi kujadili
nani awekeze, upatikanaji wa mikopo itakuwaje na mambo mengi
yanayohusiana,” alisema.
Serikali iliwahi kulieleza Bunge wakati
ikijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Aprili 2007
kuwa suala hilo ni la kisera kwa kuwa wawekezaji wameruhusiwa na
Serikali ilikwishajitoa kwenye biashara.
Akijibu swali hilo
ambalo Lembeli alitaka kujua kwa nini mtambo huo usijengwe nchini,
aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Lawrence Masha alisema hali
hiyo imetokana na Serikali kukosa wawekezaji au wawekezaji kuchelewa
kufanya hivyo hapa nchini.
Masha alilishauri Bunge lishirikiane
na Serikali kuendelea kuwakaribisha na kuwashawishi wawekezaji kuja
kuwekeza katika mtambo huo wa kuchenjua mchanga, akibainisha kuwa
uwekezaji huo unahitaji mtaji mkubwa.
Miaka kadhaa iliyopita,
aliyekuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi, Uzalishaji na Biashara ya Madini wa
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Liberatus Chizuzu alikaririwa akisema kuwa gharama za
uwekezaji wa mtambo huo ni kubwa ikilinganishwa na thamani ya mapato
yanayopatikana kupitia uchenjuaji wa madini yaliyopo.
Chizuzu
alisema miongoni mwa masharti ya uwekezaji wa mtambo huo ni upatikanaji
wa umeme wa uhakika, jambo ambalo ni changamoto hapa nchini.
Lisu ampa somo
Juzi, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alitoa angalizo
kuhusu hatua hiyo ya Rais akisema Kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao
wanalindwa kisheria na kimkataba.
Mwanasheria huyo mkuu wa
Chadema alisema kwa mujibu wa Sheria ya Madini na Mikataba ya
Uendelezaji Madini (MDA), madini yote yanayochimbwa ni mali ya
wawekezaji.
Alisema kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao
wanalindwa kisheria na kimkataba, hatua hiyo inaweza kuwafanya
wawekezaji hao kwenda mahakama za usuluhishi za kimataifa.
Alisema
Rais alitakiwa kufanya kama mwenzake, Evo Morales wa Bolivia ambaye
nchi yake ilikuwa na mikataba kama ya Tanzania lakini alipochaguliwa
Desemba, 2006 aliiondoa kwanza kwenye mikataba hiyo iliyokuwa
inailazimisha kuingia kwenye migogoro ya uwezekaji na baada ya hapo
ndipo akabadilisha sheria na mikataba ya uwekezaji iliyoipa Bolivia
sehemu kubwa ya umilikaji wa gesi na mafuta ya nchi yake.
Post a Comment