Siku 135 tangu Valentino Mlowola alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu
wa Takukuru tayari ana kesi kubwa zipatazo 30 zinazosubiri uchunguzi zikiwamo
zilizoibuliwa na Rais John Magufuli.
Januari
26, Mlowola ambaye alithibitishwa kuwa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo Machi
mwaka huu alieleza mikakati yake ya kutumbua majipu akianika kesi kubwa
zinazoshughulikiwa na taasisi hiyo, zikiwamo zilizokamilika na kupelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kuombewa kibali cha kuwafikisha
mahakamani waliobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Alipoulizwa
kama Takukuru itaweza kukamilisha uchunguzi wa kesi hizo, mkurugenzi huyo wa
zamani wa Intelijensia ya Jinai katika Jeshi la Polisi alisema: “Hatuwezi
kuacha kuchunguza kwa sababu ya muda na tunawalipa watumishi wetu kwa sababu ya
kazi hii ya uchunguzi. Tuna watumishi wa kutosha ndiyo maana tunachunguza kesi
nyingi.”
Baadhi ya
kesi kubwa zinazochunguzwa na Takukuru ni ile ya kampuni ya Lugumi
inayotuhumiwa kulitapeli Jeshi la Polisi, utakatishaji wa fedha uliotajwa
kwenye ripoti ya Panama Papers, tuhuma za rushwa kwa wabunge, madai ya Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kushawishiwa kupewa
rushwa.
Nyingine
ni sakata la kampuni ya Lake Oil kukwepa kodi ya Sh8.5 bilioni, ununuzi wa
mabehewa feki 25 na ukiukwaji wa taratibu za kuwapata wazabuni, matumizi mabaya
ya fedha yanayodaiwa kufanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na
tuhuma mbalimbali zinazowakabili waliokuwa vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Lugumi
Takukuru
inachunguza sakata la kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh37 bilioni na
Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole
nchi nzima.
Kampuni
hiyo inadaiwa kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu
kati ya 106 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha
kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua
udhaifu huo.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi
juzi alisema Takukuru inashughulikia suala hilo, huku akibainisha kuwa kwa sasa
Brela haina takwimu za kina za kampuni hiyo.
Utakatishaji
fedha
Takukuru
pia inawachunguza waliohusika na utakatishaji fedha wakati Serikali ilipokopa
Dola 550 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.1 trilioni) kutoka Benki ya Standard
ya Uingereza.
Tayari
watu watatu; Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry
Kitilya, pamoja na maofisa wawili waandamizi wa zamani wa Benki ya Stanbic (T),
Shose Sinare na Sioi Solomon, wameshafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
kwa makosa manane likiwamo la kutakatisha fedha.
Takukuru
iliwahi kukaririwa ikisema kila aliyetajwa katika sakata hilo kama
ilivyoripotiwa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO),
anachunguzwa ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo, lakini
hakutaja majina yao.
Katika
hilo la kutakatisha fedha, Takukuru imejitosa kufuatilia ripoti ukwepaji kodi
ya Panama Papers ili kubaini kama kuna Watanzania waliohusika.
Kashfa
hiyo inayotikisa dunia kwa sasa inahusisha nyaraka zilizoibuliwa na mtandao wa
waandishi wa habari ambazo zinawafichua watu maarufu duniani, wakiwamo wakuu wa
nchi 12 walioko madarakani na waliostaafu, familia na marafiki zao wa karibu
ambao wamenufaika na ukwepaji kodi.
Takukuru
ilieleza kuwa Watanzania watakaobainika kutajwa katika ripoti hiyo
watachukuliwa hatua kulingana na sheria za nchi.
Matukio
mengine
Takukuru
pia ilitangaza kuanza kuchunguza taarifa zilizotolewa na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuwa alishawishiwa kupokea rushwa
ya Sh5bilioni na wafanyabiashara wakubwa huku ikiichunguza kampuni ya Lake Oil
inayotuhumiwa kuingiza kwenye soko la ndani lita milioni 17.4 za mafuta
yaliyotakiwa kwenda Congo hivyo kukwepa kodi ya Sh8.5bilioni.
Kesi
nyingine kubwa inayofuatiliwa na Takukuru ni ile ya ununuzi wa mabehewa 25 ya
mitumba uliokiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma namba 21/2004 kutoka kampuni ya
Hindustha Engineering and Industries Limited. Nyingine ni ile inayomhusu
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Hodhi la Rasilimali za Reli (Rahco),
Benhadard Tito baada ya kubaini kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na
taratibu za kuwapata wazabuni kwenye mradi wa ujenzi wa reli.
Mtihani
mwingine wa Takukuru ni juu ya uchunguzi wa tuhuma za kuomba rushwa
zinazowakabili baadhi ya wabunge. Mpaka sasa wabunge takribani 10 wameshahojiwa
na taasisi hiyo, akiwamo wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na wa Nzega Mjini,
Hussein Bashe ambao walimuandikia Naibu Spika Job Ndugai, barua za kujiuzulu
katika kamati zao ili kupisha uchunguzi huo.
Tayari wabunge
kadhaa wameshafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashtaka ya kuomba rushwa ya Sh30milioni. Hao ni Ahmad Saddiq (Mvomero), Kangi
Lugola (Mwibara) na Victor Mwambalaswa (Lupa)
S0urce mwananchi
Post a Comment