Spika John Ndugai
amefanya mabadiliko ya wajumbe 27 wa Kamati za Kudumu za Bunge yaliyowang’oa
wenyeviti watano, huku mmoja akipoteza nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bunge.
Hatua hiyo imekuja wakati
kukiwa na tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge wa baadhi ya kamati na kusababisha
baadhi kujiuzulu ujumbe wakishinikiza uchunguzi ufanyike ili waliohusika
wawekwe hadharani na kuchukuliwa hatua.
Taarifa iliyotolewa na
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliacho cha Bunge inasema Spika Ndugai
amefanya mabadiliko hayo kwa kuzingatia mahitaji mapya na changamoto
zilizojitokeza baada ya kuunda kamati hizo siku 59 zilizopita.
Waliong’olewa uenyekiti
ni Richard Ndassa, ambaye alikuwa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), Dk Mary
Mwanjelwa (Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira), Martha Mlata (Kamati ya
Nishati na Madini).
Waliovuliwa umakamu
mwenyekiti ni Dk Raphael Chegeni (Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii) na
Kangi Lugola (Kamati za Hesabu za Serikali).
“Mabadiliko haya
yamefanywa chini ya Kanuni ya 116(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo inatoa
mamlaka ya kuteua wabunge kuunda kamati mbalimbali za Bunge,” inasema taarifa
hiyo.
Kwa kuhamishwa kutoka
kamati wanazoziongoza, wabunge hao wamepoteza nafasi zao za uenyekiti, wakati
Mwanjelwa, ambaye alipata nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge kutokana na kuwa mmoja
wa wenyeviti wa kamati hizo, amepoteza wadhifa huo wa kuwa mmoja wa wenyeviti
watatu ambao humsaidia Spika kuongoza shughuli za Bunge.
“Sifahamu chochote,”
alisema Dk Mwanjelwa, mmoja wa wenyeviti watatu wa Bunge, alipoulizwa na
Mwananchi kuhusu mabadiliko hayo.
“Ninachoweza kusema
uamuzi wa Spika ndiyo wa mwisho, ila sina ninachofahamu kuhusiana na mabadiliko
haya. Yaani ndiyo nimesoma kwenye mtandao muda si mrefu kabla hamjanitafuta.”
Taasisi za Serikali
zinazotuhumiwa kutoa fedha kwa wajumbe wa Kamati za Bunge, ambazo zina jukumu
la kuzisimamia, ni Shirika la Nyumba (NHC), Bima ya Afya (NHIF), Shirika la
Umeme (Tanesco) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Meneja Mawasiliano na
Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema suala la taasisi yake kutoa rushwa kwa
wabunge limewashangaza, na wanasubiri vyombo vya uchunguzi kutoa matokeo kuhusu
tuhuma hizo.
“Matokeo ya uchunguzi
kuhusu tuhuma hii ndiyo ambayo yanaweza kuanika bayana kama kweli tunahusika au
lah. Ni jambo ambalo hata sisi limetushangaza,” alisema.
Kutokana na mabadiliko
hayo, kamati ambazo viongozi wake wameondolewa zitalazimika kufanya uchaguzi wa
viongozi.
Kamati zinazotakiwa
kupata wenyeviti wapya ni ya Nishati na Madini, Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo itatakiwa kufanya uchaguzi wa
mwenyekiti na makamu wake, wakati zitakazochagua makamu ni ya Hesabu za
Serikali ya Mitaa (LAAC) na ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Waliohamishwa wazungumza
Akizungumzia suala hilo,
Dk Chegeni alisema wajumbe wawili wa kamati yake, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na
Hussein Bashe (Nzega Mjini), wamemuandikia Spika barua za kujiondoa kwenye
nafasi zao ili kupisha uchunguzi wa rushwa.
“Wajumbe wa kamati
wamesikitishwa na taarifa hizi na kwa pamoja tumeamua kuchukua hatua.
Tumemuandikia Spika barua ya kupisha uchunguzi ili kujiridhisha na madai
yaliyobainishwa. Wajumbe wote waliohudhuria kikao cha leo wamesaini,” alisema
Dk Chegeni.
Zitto aliiambia Mwananchi
kuwa amemuandikia Spika barua ya kujiondoa, akitaka uchunguzi ufanyike na
atakayehusika achukuliwe hatua kali.
Bashe alithibitisha kujiondoa
akitaka uchunguzi ufanyike na watuhumiwa wote watajwe kwa majina ili hatua
zichukuliwe.
“Utumishi wangu kwa
kamati uko palepale nisingependa kuhamishwa lakini watuhumiwa wajulikane,”
alisema Bashe.
Akizungumzia taarifa
zilizochapishwa na gazeti moja jana, Dk Chegeni alisema: “Si kweli. Hata huyo
katibu anayeelezwa kutumwa hakuwa nasi mpaka mwisho wa ziara pale Bima ya Afya.
Alitoa udhuru kuwa mwanaye anaugua na akaruhusiwa kuondoka mapema tu. Leo
(Jana) kamati imewauliza wajumbe na makatibu wote na wamekana kuhusika.”
Baada ya kujiridhisha na
kutohusika kwa wajumbe wake, Dk Chegeni alisema kamati imepitisha maazimio
matatu, ambayo ni kutaka uchunguzi ufanyike ili ofisi ya Spika ijiridhishe,
watakaobainika wachukuliwe hatua za kikanuni na kisheria, na gazeti
lililoandika habari hiyo lithibitishe tuhuma hizo na likishindwa liiombe
msamaha kamati.
“Jana (juzi) nilitumwa na
mwenyekiti wangu nihudhurie kikao Spika kilichokuwa kifanyike saa 5:00 asubuhi,
lakini kiliahirishwa. Leo (jana) hajahudhuria kikao chetu na kanijulisha kuwa
anahudhuria kikao hicho kikichoahirishwa jana (juzi). Sina taarifa za mahojiano
na Takukuru,” alisema Lolencia Bukwimba akimzungumzia Ndassa.
Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi alisema hajajiuzului ujumbe wa kamati kama habari zilivyoenea,
lakini yeye pamoja na wajumbe wenzake wa Kamati ya Huduma za Jamii wamemtaka
Spika awaeleze kilichotokea kwa kuwa ndiye kiongozi wao.
“Kwa mfano mimi nijiuzulu
nini wakati si mtuhumiwa?” alihoji.
“Nikijiuzulu, maana yake
naacha kazi za kibunge.”
Alisema anashangaa habari
kama hizo zinatokea wapi wakati hajasikia kama kuna mbunge yeyote aliyehojiwa
dhidi ya tuhuma hizo.
Kuhusu tuhuma za rushwa,
Mbilinyi alisema si rahisi kwa kitu hicho kutokea kwa kuwa wabunge hawawezi
kuwatuma makatibu wa kamati kufuata fedha za rushwa.
“Kwa sababu huwa
tunawaona kama wapelelezi, hivyo si rahisi mtu akamuamini kiasi cha kumtuma
akamchukulie mzigo,” alisema.
Pia alisema kwa wakati
huu ambao Bunge ni changa, haiwezi kuwa rahisi wakakubaliana kuchukua rushwa
kwa kuwa bado wabunge hawajafahamiana vizuri.
Mbunge wa Jimbo la
Bukene, Selemani Zedi alisema hajapata taarifa rasmi za kuhamishwa kutoka
kamati ya PIC kwenda ya Katiba.
“Nitawajibika kwenye
kamati nitakayopangwa kwa sababu spika anayo mamlaka ya kunipanga popote,”alisema.
Kuhusu vitendo vya
rushwa, alivitaka vyombo husika kufanya uchunguzi ili atakayebainika kuhusika
achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Mwaka 2012, wajumbe wa
Kamati ya Nishati na Madini walituhumiwa kupokea hongo kutoka kwenye makampuni
ya mafuta ili waunge mkono azimio la kushinikiza aliyekuwa katibu mkuu wa
wizara husika, Eliackim Maswi ang’olewe.
Wakati huo, Spika Anne
Makinda aliahidi kuwapeleka watuhumiwa kwenye Kamati ya Maadili na Haki za
Bunge ili wachunguzwe na kuahidi kuwa matokeo ya ripoti hiyo angeiwasilisha
bungeni.
Siku hiyo, Spika Makinda
pia alitangaza kuivunja kamati ya nishati.
Imeandikwa na Tumaini
Msowoya, Julius Mathias na Elizabeth
Post a Comment