Wakati Serikali ikikosa majibu juu ya vifo vya kutatanisha vya watu
wawili waliofariki kwa dalili za ebola, miili ya watu hao imezikwa jana na
O
fisi ya Mganga Mkuu wa Serikali kwenye makaburi ya Mwananyamala.
Hatia hiyo imechukuliwa ili kuepusha kuenea kwa ugonjwa huo ambao
mpaka sasa haujafahamika na sampuli za damu zimepelekwa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa
ya Kenya (KEMR) kwa uchunguzi zaidi.
Jana, ndugu wa marehemu walikusanyika katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) kwa ajili ya mazishi hayo ambayo yalifanywa na Serikali kwa
asilimia 100 kwani walitakiwa kukaa mbali bila kusogelea kaburi, kuaga wala
kugusa majeneza.
Watu hao walifariki kati ya Machi 16 na 20 katika hospitali hiyo
wakipata matibabu baada ya kupata homa kali na kutokwa damu sehemu mbalimbali
za miili yao ikiwamo kwenye ngozi.
Mwandishi wetu alishuhudia msafara wa mazishi hayo uliojumuisha
basi lililobeba ndugu wa marehemu wote wawili na kutanguliwa na gari maalumu la
Serikali lililobeba wataalamu wa afya na gari la tatu lilibeba miili hiyo. Pia,
katika gari hilo lenye rangi nyeupe, walikuwamo wataalamu saba wa afya
waliokuwa wamevalia mavazi meupe ambayo aghalabu hutumiwa wakati wa kuhudumia
wagonjwa wa ebola au homa ya bonde la ufa.
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Juma Seromba alisema baada ya Serikali
kuamua kuizika miili hiyo, waliamua kuupeleka msiba Iringa.
“Kwa kuwa Serikali imeshaamua hatuna la kufanya, naamini wana nia
njema na afya zetu lakini sisi tunachosubiri ni kujua aina ya ugonjwa uliomuua
ndugu yetu,” alisema.
Akiwa ndani ya basi tayari kwa kuelekea kwenye mazishi, mmoja wa
ndugu wa marehemu kutoka Kilimanjaro, Nicholaus Msuya aliilaumu Serikali kwa
uamuzu huo.
“Wametuambia dakika za mwisho kuwa hatutaweza kumzika dada yetu kwa
sababu ana dalili za ebola. Tulitaka kuusafirisha mwili lakini daktari kazuia.
Hatuna cha kufanya,” alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa MNH, Dk Praxeda Ogweyo
alisema hakuna mgonjwa mwingine aliyefikishwa hospitalini hapo akiwa na dalili
hizo.
“Bado idadi ya wagonjwa waliofariki ni walewale wawili hakuna
ongezeko, lakini bado tunasubiri majibu ya vipimo kutoka Kenya, ndipo tutajua ni
ugonjwa gani,” alisema.
Wiki iliyopita Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema vipimo vya
awali vilivyofanyika nchini havijagundua aina ya ugonjwa uliosababisha vifo
hivyo.
Ripoti ya hivi karibuni kutoka Shirika la Habari la Uingereza
(Reuters) inaonyesha kuwa zaidi ya watu 60 wamefariki dunia Angola kwa dalili
kama hizo na baadaye kubainika kuwa ilikuwa ni homa ya manjano (yellow fever).
Kadhalika, watu wawili wameripotiwa kufariki dunia huko Kenya kwa homa ya
manjano huku mmoja kati yao akibainika kuwa alitokea Angola.
Post a Comment