Zikiwa zimebaki
siku chache kabla ya kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar, Makamu
wa Kwanza wa Rais
Maalim Seif Sharrif Hamad amehoji sababu za chama tawala, CCM kuhofia CUF
kuongoza visiwa hivyo. Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 ambao matokeo yake yalifutwa, pia amesema endapo CCM itasitisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika siku 36 zijazo, CUF watakuwa tayari kufanya mazungumzo lakini si kwa wakati huu ambao maandalizi ya kupiga kura yanaendelea.
Akizungumza na waandishi
wa habari jana, katibu huyo mkuu wa CUF aliitoa hofu CCM kuwa chama chake
hakina ajenda ya kulipiza kisasi.
Matokeo ya uchaguzi wa
Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha siku ambayo chombo hicho kilitakiwa
kumtangaza mshindi, na mwezi uliopita alitangaza Machi 20 kuwa siku ya uchaguzi
wa marudio visiwani humo.
Wakati CUF ikipinga
vikali kufutwa matokeo na kutangaza tarehe mpya, Serikali imesema kuna nafasi
ya kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna muda
mrefu wa kufanya hivyo.
Jecha alitangaza uamuzi
huo wakati tayari matokeo ya urais ya majimbo 31 yalishatangazwa, na ya majimbo
tisa yaliyosalia yalishahakikiwa, huku washindi wa viti vya uwakilishi na
udiwani wakiwa wametangazwa na kupewa vyeti vya ushindi.
“Sijui kwa nini CCM
wanaogopa sisi tukiongoza?” alihoji Maalim Seif kwenye
mkutano huo na waandishi akiwa pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
“Wana wasiwasi gani,
kwamba CUF ikiongoza kutatokea nini? Sisi hatuna ajenda ya kulipiza kisasi,” alisema.
Katika mkutano huo,
Maalim Seif mbaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho alisema kama CCM ina
wasiwasi na idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye Serikali ya Umoja
wa Kitaifa (SUK), haina budi kuondoa shaka kwa kuwa idadi kwa pande zote
inakaribiana.
“Hawa wanahisi hawatapata
uwakilishi mkubwa, lakini mbona miaka yote tunakuwa na idadi isiyopishana ya
wawakilishi?” alihoji.
Kuna Vitisho
Zanzibar
Katika mkutano huo,
Maalim Seif alisema kumekuwapo vitendo vya wananchi kupigwa na vikundi vya watu
wasiojulikana.
Alidai wafanyakazi wa
Serikali na taasisi zake wameamrishwa kupeleka vitambulisho vyao vya kazi na
vya kura serikalini ili vikahakikiwe.
“Hii si mara ya kwanza
wafanyakazi wa Serikali kutakiwa kupeleka vitambulisho, sisi tunajua kuwa
wanataka wawatishe kuwa watajua nani kapiga kura na nani hajapiga,” alisema
na kusisitiza:
“Hii ni kama kitisho cha
kuwalazimisha wakapige kura, zaidi hasa hizo ni dhuluma ambazo wananchi
wanafanyiwa.”
Kadhalika Maalim Seif
alizungumzia uwapo wa watu wanaovaa soksi usoni na kuwashambulia raia, akisema
Serikali haijachukua hatua stahiki kudhibiti hali hiyo.
Alisema watu hao ambao
wamepachikwa jina la mazombi, wamevamia maeneo kadhaa kama Baraza la CUF, Jang’ombe
na yaleambayo yana wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo.
“Wanawapiga watu,
wanawajeruhi na wanaiba mali, lakini inashangaza sana mambo haya na si Serikali
wala polisi iliyochukua hatua,” alisema.
Maalim Seif alisema
amezungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuhusu matukio hayo ya
uharamia wanaofanyiwa wananchi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
Alisema CCM wanatafuta
sababu ili machafuko zaidi yatokee visiwani humo wapate kisingizio.
Aliwataka wafuasi wa CUF
kuvumilia hali hiyo ili nchi isiingie kwenye machafuko kama yaliyotokea mwaka
2000, wakati watu zaidi ya 20 waliuawa na wengine kukimbilia Shimoni, Mombasa
nchini Kenya ambako waliishi kama wakimbizi.
Lowassa Azungumza
Kwa upande wake, Lowassa
aliwataka viongozi wa ngazi za juu wachukue hatua kumaliza mgogoro
wa Zanzibar.
“Hili tulichukulie kwa
umakini sana. Viongozi wafanye vikao vya maridhiano, tunaipenda sana amani
tuliyonayo,” alisema.
Lowassa alisema
anashangazwa na jinsi CCM wanavyoshindwa kuheshimu makubaliano ya SUK na
kukataa kukubali matokeo.
ZEC yagoma
kuondoa picha ya Maalim
Wakati huohuo, habari
zinaarifu kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar( ZEC)
imegoma kuondoa picha za wagombea
Urais,Udiwani na Uwakilishi kutoka vyama
vilivyotangaza kutoshiriki uchaguzi wa
marudio,ikiwemo jina na picha Maalim Seif Sharif Hamad.
Hilo
lilifahamika jana mjini Unguja baada ya kigogo
mmoja wa ZEC ambaye hakuwa tayari kutaja
jina kusema kuwa sheria hazimruhusu mgombea
yeyote kujitoa mwenyewe kwa utashi wake
binafsi.
Kiongozi huyo
alisema kwa mujibu wa kifungu cha 36
cha sheria ya uchaguzi namba 11 ya
mwaka 1984,mgombea hawezi
kujiondoa kwa utashi wake baada ya
Tume kukamilisha kazi ya uteuzi ambayo
ilifanyika kabla ya Oktoba 25 mwaka jana.
"Ieleweke
kwamba mgombea urais anaweza kujiondoa katika
kinyang'anyiro kwa kuwasilisha taarifa za
maandishi yeye mwenyewe ofisi za ZEC
kabla ya saa 10 jioni ya siku ya
uteuzi."Alisema ofisa huyo akinukuu
kifungu cha katiba.
Alisema
uteuzi wa mgombea mwingine unaweza
kufanyika ndani ya siku 21 kama mgombea
hatafariki dunia,lakini hakuna ruhusa ya kujitoa
kabla ya kukamilika kwa uchaguzi.
Alisema ZEC
tayari imeviandikia vyama kuvitaka vithibitishe iwapo
wagombea wao wangali hai au kuna
waliofariki dunia, na si kutaka kufahamu kama
watashiriki uchaguzi wa marudio au la.
Mkurugenzi wa
Mipango na Uchaguzi CUF anena
Mkurugenzi wa
Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe amesema
ZEC inasuka mkakati wa siri wa kutaka
kuzitumia picha na taarifa za wagombea wao
kwa lengo la kuidanganya dunia na
jumuiya za kimataifa kwamba CUF walishiriki
uchaguzi huo.
Shehe amesema
CUF kilitangaza mapema kabisa kutoshiriki
uchaguzi wa marudio,hivyo dunia nzima
inaelewa kabisa kwamba CUF haishiriki
uchaguzi huo na kitendo cha kuendelea
kuchapisha picha na taarifa za wagombea
wao katika karatasi za wapiga kura si
sahihi.
Post a Comment