Mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahim Kaduma amemshauri Rais John
Magufuli kurejesha nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watu binafsi wengi wao
wakiwa waliokuwa watumishi wa umma, akisema ndiyo njia ya “kujisahihisha”.
Kaduma, ambay
e amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya
Awamu ya Kwanza, aliyasema hayo wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na
gazeti hili kuhusu mambo kadhaa juu ya mwenendo wa CCM na Serikali yake katika
kipindi ambacho chama hicho kimeadhimisha miaka 39 tangu kianzishwe.
“Kitu muhimu ambacho namshauri Rais, ni kuzirudisha nyumba za
Serikali. Uuzaji wake haukuwafurahisha Watanzania walio wengi. Asimamie
urudishaji huo ila afanye hivyo baada ya kutunga sheria ya maadili ya utumishi
wa umma,” alisema.
Nyumba hizo za Serikali ziliuzwa wakati wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa kwa usimamizi wa Dk Magufuli wakati huo
akiwa Waziri wa Ujenzi.
Alimtaka Rais Magufuli kurejea kitabu kilichoandikwa na Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere cha ‘Tujisahihishe’ kwa yeye mwenyewe kuanza
kujisahihisha kwa kurejesha nyumba ya Serikali aliyoinunua kwa utaratibu ule.
Alishauri kabla ya kufanya hivyo, Rais Magufuli atengeneze Sheria
ya Maadili ya Taifa ambayo itamwambia kila mmoja amwogope Mungu na aseme ukweli
wa mali wanazomiliki jinsi walivyozipata.
“Tujisahihishe maana yake kwa kiroho ni kutubu, Magufuli yeye
mwenyewe angeanza kwa kutubu kwa wananchi, aeleze wazi kuwa CCM iliwakosea
Watanzania (katika suala la uuzaji wa nyumba za Serikali).
Kuhusu CCM
Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje, alisema ili CCM iendelee
kushika dola, haina budi kuirudia misingi iliyowekwa na waasisi wake ambayo
imeachwa.
Alibainisha kuwa chama hicho kilirithi misingi ya vyama vya
ukombozi vya Tanu na ASP, hivyo kinatakiwa kujitathmini kama kinatekeleza
matakwa yaliyokusudiwa ya kuwakomboa Watanzania na kuwawezesha kupiga hatua ya
maendeleo kwa wakati na kujikwamua kiuchumi.
“Taasisi yoyote yenye dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi wake
ni lazima iwe na utamaduni wa kujitathmini. CCM ya sasa imepotoka na kusahau
misingi yake. Endapo itarudi na kuisimamia, basi itatawala kwa muda mrefu
ujao,” alisema.
Kaduma alisema kwa miaka kadhaa iliyopita, Taifa limesahau maadili
ya uongozi na kujikuta likiyafumbia macho mambo yasiyofaa hasa yanapofanywa na
viongozi wa Serikali.
Alitoa wito kwa wenye dhamana ya uongozi, kwa nafasi zao,
kukubaliana juu ya maadili na misingi ya Taifa ili kwa pamoja, kusukuma
gurudumu la maendeleo.
“Nchi hii tumeheshimu unafiki kuliko ukweli kwa kusahau maadili na
misingi. Ni lazima tukae kama Taifa na tukubaliane juu ya namna tutakavyoiongoza
nchi yetu,” alisema.
Kubana matumizi
Wakati Rais Magufuli akikaribia kutimiza siku 100 tangu aingie
madarakani, Mzee Kaduma aliwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono akisema
tayari ameonyesha kuwajali na kuwafanyia kazi kama alivyoahidi.
Alisema amejitahidi kubana matumizi ya Serikali, kuongeza
ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma za jamii jambo ambalo mbali na
kurejesha heshima ya nchi, litasaidia kuwapunguzia Watanzania umaskini.
“Kufuta safari za nje kwa watendaji wa Serikali kumewaudhi wengi
kwa sababu walikuwa wanalipana fedha nyingi sana. Lakini hivi ndivyo
tulivyoishi enzi za Mwalimu. Magufuli hana makuu na anawatetea wanyonge,
nawaomba sana Watanzania tumuunge mkono.”
Mabadiliko ya sheria
Akizungumzia majukumu ya mkuu wa nchi katika utekelezaji wa utawala
bora na demokrasia, Mzee Kaduma alisema ipo haja ya kufanya marekebisho katika
baadhi ya sheria.
Alisema ni wakati muafaka sasa wa kuirekebisha Sheria ya Uchaguzi
ili kutenganisha majukumu ya kiserikali na kichama kwa Rais.
“Tunahitaji Rais huru ambaye hatakuwa na minyororo ya chama chake
ili atuongoze kwa umoja wetu. Yafaa matakwa ya mgombea kutokana na chama cha
siasa yaondolewe ikiwa ni pamoja na kuzuia Rais kuwa mwenyekiti wa chama. Endapo
Rais atakuwa huru, ataweza kuwaita wenyeviti wa vyama na kuzungumza nao bila
upendeleo wowote,” alisema.
Pamoja na maoni hayo, alisema hana shaka na uongozi wa Rais
Magufuli. “... Anafanana na Mwalimu Julius Nyerere. Wote wanawajali maskini na
walifanya kila wawezalo ili kuwakomboa kutoka kwenye minyororo yote iliyofunga
uhuru wao, iwe kiuchumi au kijamii, ili kuwafanya wafurahie rasilimali za Taifa
lao.”
Mgogoro Zanzibar
Kaduma aliungana na wadau wengine ambao wanapinga kurudiwa kwa
uchaguzi wa Zanzibar kwa maelezo kuwa maridhiano baina ya pande zinazosigana
yana nafasi nzuri ya kutatua mgogoro uliopo.
“Katika suala la Zanzibar nadhani CCM tungekubali kushindwa. Mimi
ni mwanaCCM lakini nasema tungekubali kushindwa. Ningekuwa (Dk Ali Mohamed)
Shein ningelinda heshima yangu maana hii ni hatari,” alisema.
Mzee Kaduma alisema kwa kuwa suala la Zanzibar ni baina ya vyama
vya CCM na CUF, mtu pekee wa kutafuta ukweli ni mwenyekiti wa CCM.
“Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiye mwenye uwezo mkubwa wa kuweka
mambo ya Zanzibar sawa maana yeye ndiye mwenyekiti wa CCM na suala lenyewe
linakihusu CCM na CUF, ingawa kwa mbali sana Magufuli naye anaweza kufanya
lolote kuondoa tatizo lililopo,” alisema.
Alisema anaamini CCM ingetenda haki kama ingepokea matokeo kama
yalivyokuwa ambayo hata waangalizi wa ndani na nje wamesema hayakuwa na dosari.
“Ni vyema Rais Shein angekubali kushindwa. Chama pia kingefanya
hivyo. Huko ndiko kujisahihisha. Kufanya hivyo Rais Shein angeondoka na heshima
yake.”
Uhuru wa habari
Kuhusu hatua ya Serikali kuonekana kuminya uhuru wa vyombo vya
habari kwa kufungia baadhi ya magazeti, Mzee Kaduma alisema: “Kama unataka
kushinda ufisadi na rushwa, ni lazima vyombo vya habari viwe huru... ila
waandike katika misingi iliyowekwa na inayokubalika kisheria.”
Akieleza jinsi vitendo vya rushwa na ufisadi vilivyotamalaki nchini
kwa miaka ya hivi karibuni, alisema ili kufanikisha suala hilo ni lazima wadau
wote washirikishwe.
Alisema suala hilo linahitaji ushiriki wa mihimili yote ya dola
bila kusahau umuhimu wa vyombo vya habari. “Vita ya rushwa na ufisadi
itapiganwa vyema endapo kutakuwa na uhuru wa habari na vyombo vyake. Kitu
muhimu ni uwapo wa sheria makini ambayo itazingatiwa na kila mmoja. Naishauri
Serikali itekeleze suala hili ili kila Mtanzania atoe mchango wake,” alisema
Post a Comment