Edwin
Semzaba, nguli wa fasihi nchini hatunaye tena. Mungu kamchukua mapema wakati
bado tunamhitaji.
Wakati
taarifa za kifo chake zikienezwa, nilikuwa namalizia kurasa za mwisho za riwaya
ya Ada
m Shafi, iitwayo ‘Mbali na Nyumbani.’
Nilikuwa
napata ‘utamu’ wa kazi za fasihi za wazee wetu, waandishi nguli ambao bado
nafasi zao hazijaonekana bayana kuzibwa na vijana wa sasa tunaojaribu kujikita
katika uandishi.
Nilikosa
maneno ya kuandika katika siku za mwanzo. Nilihisi sitaweza kuandika chochote
cha maana na cha kina juu yake, kwa kuwa mimi ni mwanafunzi wake kama wengine,
tulionufaika na tunaoendelea kunufaika na kazi zake.
Kibaya
zaidi, sikuwa namfahamu kama wazee wenziwe au wafanyakazi aliyefanya nao zaidi
ya uelewa mdogo kupitia kazi zake kama ‘Sofia wa Gongo la Mboto’ na ‘Ngoswe
Kitovu cha Uzembe’, tamthilia ambayo wengi tuliisoma tukiwa sekondari.
Hata
hivyo, picha zake nilizozikuta kwenye kamera yangu wakati nataka kuzifuta
nisizohitaji, ziliniongezea huzuni na kujikuta nakumbuka maandishi yake na
kikubwa kuuwazia mustakabali wa fasihi andishi nchini.
Shukrani
kwa mwandishi mwenzangu Edward Qorro, ambaye aliitumia kamera yangu kumpiga
picha Semzaba wakati akifanya naye mahojiano na nakala kubaki katika kifaa
hicho ambazo zitabaki kuwa kumbukumbu.
Semzaba
amefariki wakati waandishi wengi maarufu wa vitabu vya fasihi nchini umri wao
ukiwa umeanza kuwatupa mkono kama ilivyo kwa babu Adam Shafi, Profesa Euphrase
Kezilahabi, Profesa Amandina Lihamba na Profesa Emmanuel Mbogo.
Semzaba
pia amefariki wakati kizazi cha sasa kinazidi kuugua ugonjwa wa kutopenda
kusoma vitabu. Kafariki wakati vijana wanasoma kwa sababu wanalazimika kusoma
ili kufaulu mitihani na siyo kupata maarifa.
Ni bahati
mbaya ugonjwa wa kutosoma vitabu unatokea wakati upatikanaji wa vitabu unazidi
kuwa rahisi kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari ya mawasiliano (Tehama).
Sehemu
kubwa ya vijana hatuna hamasa tena ya kusoma vitabu, licha ya ukweli kwamba
tunakesha tukisoma taarifa za kwenye mitandao ya kijamii.
Muda
unaotumika kupiga soga katika mitandao hiyo kwa jumla huenda ukawa hata robo ya
siku nzima, lakini kusoma kazi za fasihi huonekana ‘zinatia uvivu’ na kufanya
watu wasisinzie. Semzaba amefariki wakati siyo tu vijana hawapendi kusoma, bali
hata kuandika ni shida. Hii ni kwa sababu asiyependa kusoma na kupata maarifa,
hukosa pia cha kuandika.
Kwa sasa
Taifa linakabiliwa na uhaba wa waandishi bora wa kazi za fasihi. Hata baadhi ya
rafiki zangu waliosoma shahada za fasihi na sanaa za maonyesho hawataki tena
kuandika na si wapenzi tena wa kusoma vitabu. Hii ni hatari.
Kuna
vijana wachache wanaoguswa kusoma na kuandika vitabu kama ilivyo kwa wale
wanaoandika vitabu vya hadithi fupi zinazouzwa kwenye mbao za magazeti, lakini
bado ubora na uchaguzi wa maudhui ni tatizo.
Sehemu
kubwa ya vitabu hivyo vimejaa maudhui ya mahaba zaidi kuliko ya kuelimisha na
kupoteza kabisa asili ya kazi za fasihi za Tanzania zilizojizolea sifa
ulimwenguni licha ya kuandikwa kwa Kiswahili.
Mbali na
maudhui, uhariri wa vijitabu hivyo pia huwa na matatizo ukionyesha wazi ni
namna gani subira na ubunifu wa kina hukosekana wakati wa maandalizi wa kazi
hizo.
Pamoja na
kwamba tunaomboleza, kifo cha Semzaba kiwe ni mwanzo mpya wa kutuamsha vijana
kusoma na kuandika vitabu kwa kuwa alianza uandishi akiwa bado kijana mdogo
Post a Comment