Hajiwezi kimapenzi juu ya CCM; wakati huo si alishatafuta tiketi
ya chama hicho kugombea ubunge Jimbo la Amani, Unguja, katika uchaguzi mkuu
2010?
Anajizongoa vipi hapo?
Ni kwa sababu tu utawala wa sheria
unakanyagwa ili kuruhusu wakubwa wa CCM kufika watakapo, lakini Jecha angekuwa
kitanzini kwa alichokifanya 28 Oktoba akiwa anakokujua huku akitelekeza wenzake
katika Tume waliokuwa kikaoni ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani
kilipokuwa kituo cha matangazo ya uchaguzi.
Hastahili kuonewa huruma. Amehujumu haki
ya wananchi kuamua watakacho, ameitia hasara serikali iliyotumia mabilioni ya
shilingi (inatajwa Sh. 7 bilioni hivi) kugharamia uchaguzi.
Jecha ni mhalifu anayesubiri siku ili
ashitakiwe. Baada ya hapo, kwa sababu ushahidi wa uhalifu aliotenda hautaki
tochi, kitakachofata ni kuadhibiwa na mahakama. Kiwango cha adhabu atakiamua
hakimu lakini gerezani itakuwa makazi yake.
Angalia sasa unayetamba ni Mzanzibari au
wewe Mtanzania wa upande mmoja unaounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
unapokuwa na serikali inayolinda mhalifu mkubwa kama huyu, unajisikiaje? Twende
mbele.
Chumbani wanawaweka, wahalifu wasishikwe,
kama vile ni kubaka, sheria isisimame, bali siku watataka, ukweli udhihirike.
Hapo patakuwa Jecha, dubwana, na wote walokosea; zombi nao watajua, wafisadi
tasogea, na roho zikapasuke, hela dhuluma patokwe. Eti nini? Dhuluma ikome.
Nchi ya nani? Watu. Watu ni nani? Umma.
Umma ni nani? Mkusanyiko wa wanadamu ndani ya nchi yao kwa ajili ya maslahi
yao, wao kama raia, na nchi yao – Zanzibar. Hapo pamekaa sawasawa. Panasomeka!
Basi Wazenjibari watu karimu, tena karimu
walotulia, hawataki upotevu, si kwa hili wala lile, milele wataka sawa, haki,
hishima, imani na uadili kusawiri. Hao ndio watu wetu, ndio watu wetu. Wetu
kwelikweli. Wetu!
Jecha ni mhalifu kama walivyo askari wa
serikali wanaojifunika vitambaa usoni na kuzunguka mitaa kwa gari za serikali
zikiwemo za KM (Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo) na MF (Kikosi cha Mafunzo).
Wanapiga wananchi, wanaharibu mali zao,
wakipambana na vitu visivyosema kama bendera za Chama cha Wananchi (CUF),
milingoti, mabenchi katika barza zao na sasa kuteketeza mikarafuu shambani.
Mhalifu kama walivyo watendaji serikalini
wanaoiba fedha za wananchi kwa visingizio vya kuandaa uchaguzi wa marudio,
uteuzi wa watendaji usonjia wala nia, na kuongezea nchi majeshi kama vile
imeingia vitani. Wafanyao au kufanikisha hayo, wote ni wahalifu tu kama
Jecha.
Huu ndio ukweli ninaoujua. Wanasheria – nakusudia
wale wanaojiheshimu kama wanataaluma wa kusaidia jamii wala sio waharibifu
wanaotumikia majizi na mavizaji demokrasia – wanajua hivyohivyo hakuwa na
mamlaka ya kisheria.
Kwanza hakuna kifungu cha sheria, pia
hakuna kikao kilichotangulia maamuzi aliyofanya. Haramu haramu haramu.
Siku hizi vikao vya Tume ya Uchaguzi
Zanzibar haviendi kikawaida. Hakuna majadiliano endelevu, bali kufanyia kazi
fikra za wanasiasa waovu zilizofikishwa na mateka wao kimaslahi.
Tume imekuwa ikipiga muhuri kuridhia yale
yanayokidhi matakwa ya CCM na Serikali, vinavyoshikwa na walewale wanaomlinda
Jecha na wanaomuelekeza Mkurugenzi wa Tume.
Mtendaji mmoja anasema hakuna mjadala
wenye mantiki na akili, vikao huendeshwa kimabavu. Utaratibu wa kuridhia mambo
kwa kupiga kura ndio staili ya kupitisha maamuzi, sio tena makamishna kuamua
baada ya kuangalia mantiki ya jambo lililowekwa mezani kufikiriwa.
Ndugu yangu siku hizi kinachofikishwa
lazima kipigiwe kura. Wanajua (wakubwa) itasimama 3-3 na Jecha akitia yake,
lazima tu kura itawalalia Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, Nassor
Khamis Mohamed na Ayoub Bakari Hamad.
Hawa makamishna wawili wa mwisho,
wanatokana na uteuzi uliofanywa kwa mashauriano na kiongozi wa upinzani.
Si hasha ukasikia bado inaaminishwa eti
uchaguzi uliharibika na ukafutwa kihalali. Uhalali wa kisheria wa ufutwaji
uchaguzi, ukajengwa baada ya ufutwaji. Mzaha, unafutaje uchaguzi wa wananchi,
ndipo utafute ridhaa ya Tume. Umajununi mtupu.
Jecha anaongoza Tume aliyoitusi
isiaminike. Yuleyule aliyeisingizia kuvuruga uchaguzi, kwa jicho lake lenye
makengeza, leo anatumika kuendesha uchaguzi wa marudio unaosaidia tu wakubwa
fulani kuibia wananchi. Haieleweki.
SOURCE MWANAHALISI
SOURCE MWANAHALISI
Post a Comment