0
TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU MKUTANO WA BUNGE ULIOMALIZIKA NA UCHAGUZI WA MEYA JIJI LA DAR ES SALAAM

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama, Salum Mwalim

amesema kuwa pamoja na manyanyaso wanayofanyiwa wabunge wa upinzani wanaotokana na vyama vinavyounda UKAWA, wawakilishi hao wa wananchi wataendelea kufanya kazi kwa bidii wakitimiza wajibu wao wa kuiwajibisha Serikali bungeni, ikiwemo kuibua ufisadi unaozidi kuatamiwa na Serikali ya CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Dar es Salaam Kaimu Katibu Mkuu amesema kuwa kauli zinazotolewa na matendo yanayofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuingilia mihimili ya bunge na mahakama na kuminya uhuru wa habari, ni dalili za wazi za hofu waliyonayo watawala ambao wanalazimika kutumia njia za kidikteta kujihalalisha kisiasa kuwa madarakani.

Akitolea mfano wa vitendo vya serikali kupeleka polisi wenye mbwa bungeni kuwadhibiti wabunge wa upinzani wanaoihoji serikali, Mwenyekiti wa Bunge kumsimamisha vikao Mbunge wa CHADEMA, Jesca Kishoa na kauli za Rais John Magufuli kuhusu kesi zilizoko mahakamani na kutisha vyama vingine, serikali yake kutozingatia katiba na sheria za nchi, Mwalim amesema kuwa ni dalili za wazi za vimelea vya udikteta.

“Suala la Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge kumsimamisha mbunge wetu Jesca Kishoa kwa sababu tu alihoji kuhusu ufisadi wa mabehewa hewa ya Mwakyembe ambao hata Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) nayo ilihoji ni kwa sababu tu katika mchango wake alizungumzia kashfa ya Escrow ambayo Chenge pia ni miongoni mwa watuhumiwa katika sakata hilo.

“Kamwe wasifikiri wabunge wetu wataacha kuweka hadharani ufisadi ambao umekithiri hapa nchini mwetu chini ya serikali ya CCM. Huyo Mwakyembe ambaye wanamlinda alikuwa Waziri wa Uchukuzi na hakuzuia makontena kupotea ama kutolewa bila ushuru bandarini. CCM ni ile ile…la kuvunda halina ubani. Wamefikia hatua wanaingiza polisi bungeni…hata madikteta kama Mussolini (Benito), Hittler (Adolf), Amin (Idd) hawakuwahi kufanya udikteta kama huo wa kupeleka mbwa na polisi bungeni kudhibiti wawakilishi wa wananchi.

“Kuingilia upangaji wa wajumbe wa kamati za kudumu za bunge, imezifanya kamati ambazo zinawajibika kuisimamia moja kwa moja serikali kuwekewa wajumbe ambao serikali inafikiri kuwa hawataweza kuwathibiti. Mfano kitendo cha kuondoa wanasheria wote nguli kwenye Kamati ya Katiba na Sheria na kuwapeleka kwenye Kamati ya Sheria Ndogo ni mkakati wa kuhakikisha kuwa miswada ya sheria haitaweza kupingwa na kamati kama ilivyokuwa kwenye bunge lililopita.

“Kamati za mahesabu yaani PAC na LAAC ambazo zinasimamiwa na Kambi ya Upinzani zimewekewa wajumbe wachache kutoka upinzani wakati kismingi ni kamati ambazo wapinzani wanatakiwa kuzisimamia.

“Kushindwa kuleta Mpango wa Maendeleo wa Miaka 5, maana yake ni kwamba Serikali inayojiita ni ya hapa kazi ilikuwa haifanyi kazi. Ilikuwa inauza sura tu, ikashindwa kutengeneza mpango wa taifa wa maendeleo na badala yake ikawataka wabunge wajadili mpango wa mwaka mmoja, kinyume kabisa na kanuni za bunge, sheria na katiba ya nchi ibara ya 63(3)(c),” amesema Mwalim.

Kaimu Katibu Mkuu pia ametoa pongezi kwa Kambi ya Upinzani inayoundwa na Wabunge wa UKAWA na uongozi wake kwa kazi nzuri waliyofanya katika mkutano uliopita kuendelea kuwa imara kutimiza wajibu wao mkubwa wa kuwa wawakilishi wa masuala na matakwa ya wananchi badala ya kuweka mbele masuala ya ‘bendera’ za vyama kama wanavyofanya wabunge wa CCM.

“Kwa mara ya kwanza sasa Kambi ya Upinzani Bungeni ina kanuni zitakazotumika kusimamia uendeshaji wa kambi ambazo zimetungwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16(4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Ni mfano wa kwanza katika Afrika. Zimetoa kipaumbeke kwa nidhamu, vikao vya kambi, vikao vya Baraza la Mawaziri Kivuli, utaratibu mzuri wa kupokea malalamiko na jinsi ya kuyashughulikia na umuhimu wa kuunga mkono msimamo wa kambi.

“Kambi imeweza kuteua wawakilishi na kupita bila kupingwa kama ifuatavyo; SADC Parliamentary Forum; Ally Salehe Ally,

Commonwealth Parliamentary Association (CPA); Tundu Lissu, Dr. Sware Semesi, Juma Hamad Omar, Pan African Parliament (PAP); David Silinde, Inter-parliamentary Union (IPU); Suzan Lyimo

Kamisheni ya Bunge; Magdalena Sakaya na Peter Msigwa.

“Pia tunatoa pongezi kwa Kiongozi wa Kambi, Freeman Mbowe kwa uteuzi wa Baraza Kivuli ambalo limesheheni mawaziri wenye weledi, uzoefu, tutaendelea kuwapa ushirikiano kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wao kikamilifu katika kuiwajibisha vilivyo serikali hii ya kutumbua majipu tu badala ya kuonesha dira na mwelekeo wa nchi,” amesema Mwalim.

Kuhusu uchaguzi wa Meya Jiji la Dar es Salaam

Kuhusu sintofahamu inayoendelea kuhusu hatima ya uchaguzi wa Meya Jiji la Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu amesema kuwa yote yanayoendelea katika kukwamisha demokrasia isichukue mkonodo wake, ambayo ni mchanganyiko wa hofu ya CCM na Serikali yake ni matokeo ya kushindwa kwa Rais John Magufuli kuonesha uongozi katika kusimamia Wizara ya TAMISEMI.

Amesema kuwa Rais Magufuli ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Wizara ya TAMISEMI hivyo ukandamizaji unaotokea katika manispaa na halmashauri zote ambazo vyama vya UKAWA vimeshinda na vinatakiwa kuongoza, unafanyika kwa sababu kuna baraka za waziri husika katika wizara hiyo inayosimamia serikali za mitaa.

“Magufuli anashindwa kutumbua jipu wizarani kwake, anaona majipu yaw engine tu. Hili kuminya demokrasia, kupidisha sheria na kanuni katika uchaguzi wa umeya na wenyeviti wa halmashauri hasa maeneo ambayo tumeshinda UKAWA, ni jipu hatari sana ofisini kwa Magufuli…wizara imeshinda. Anaona udhaifu wa wenzake wa kwake anaficha,” amesema Mwalim.

“Tunawaambia CCM na Magufuli na serikali yao kuwa uchaguzi ni suala la namba. Namba za ukweli zinaonesha wala hazidanganyi. Tutawashinda Umeya wa Dar es Salaam, iwe mchana iwe usiku, liwe linawaka iwe inanyesha. Wanajua hilo ndiyo maana wanaahirisha kila siku bila sababu wakitafuta namna ya kuibeba CCM. Hilo hatutalikubali.

“Ilala wanataka kuongeza wajumbe 3 kutoka 54 sasa orodha tunaletewa wako 57. Kinondoni ambako wapiga kura wakiwemo wale mawaziri walioteuliwa na rais, orodha ilikuwa watu 58, sasa wanataka kuwaongeza wafike 69. Majina yasiyokuwa halali yamechomekwa chomekwa. Hili halitakubalika. Anayebariki haya ni Magufuli, waziri mhusika wa TAMISEMI,” amesema Kaimu Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa ili mtu ahesabiwe kuwa mpiga kura halali katika uchaguzi wa Umeya wa Jiji la Dar es Salaam, kanuni zinasema wazi kuwa lazima awe mjumbe halali wa mojawapo ya manispaa zinazounda jiji hilo, yaani Ilala, Kinondoni na Temeke jambo ambalo wakurugenzi wa manispaa za Ilala na Kinondoni wakishirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na CCM, wanataka kulivunja kwa ‘kuingiza’ wapiga kura wasio halali kutoka Zanzibar.

Amemtaka Rais Magufuli kama Waziri mwenye dhamana katika Wizara ya TAMISEMI, kutoa boriti kwenye jicho lake kabla hajaanza kuondoa kibanzi kwa wengine na kwamba kuendelea kuwahimiza viongozi wa dini kuwa aombewe wakati anapindisha sheria na kanuni zilizo wazi ni kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Kuhusu kauli za Rais Magufuli

Aidha Kaimu Katibu Mkuu akijibu maswali ya waandishi wa habari, amesema kuwa kauli za Rais Magufuli aliyoitoa mbele ya wanasheria, kuhusu kesi zinazohusiana na ukwepaji kodi kuwa zina thamani ya shilingi 1 trilioni na yuko tayari kuipatia Mahakama kiasi cha 250 bilioni kama zitahukumiwa haraka ziishe, tafsiri yake ni sawa na kusema kuwa Mahakama imepewa rushwa ili serikali iweze kuzishinda kesi hizo.

“Na kama serikali ikishindwa basi Mahakama isiweze kudai fedha za miradi ya maendeleo. Ndiyo maana siku zote msimamo wetu umekuwa lazima Mahakama iwe huru, itengewe fedha kwenye mfuko maalum wake kama ambavyo mhimili wa Bunge umetengewa fedha zake za kujiendesha. Sio kama ilivyo sasa ambapo Mahakama inaenda kupiga magoti kwa mhimili wa serikali ili iweze kupatiwa fedha.

“Hatuna uhakika kama alipata ujasiri wa kuomba radhi kwa Jaji Mkuu kuwa alikosea au iwapo Jaji Mkuu alipata ujasiri wa kuwaambia majaji wake kuwa alichosema rais si sahihi. Wakati akisema hayo Dar es Salaam, alipoenda Singida kwenye sherehe ya CCM akaishiwa hoja na kuishia kuwatisha wananchi wake wanaoamini katika vyama vingine eti visahau kutawala nchi hii.

“Maana yake alikuwa anatoa maelekezo kwa vyombo vya dola kwamba hataki au hawataki vyama vingine vishinde. Ni kauli ya ajabu sana kutolewa na rais anayesema anaamini katika demokrasia na kuwa ni rais wa wote. Kuingilia mihimili mingine ya serikali na kauli kama hizo ni vimelea vya udikteta tu,” amesema Mwalim.

Imetolewa leo Jumatatu, Februari 8, 2016 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Post a Comment

 
Top