0



Serikali  imeshindwa kutoa majibu yanayoeleweka baada ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kutaka kujua ni lini serikali itakamilisha ahadi yake kwa kupeleka mada
wati 708 yaliyotokana na chenji ya rada katika kila wilaya. Anaandika Danny Tibason, Dodoma … (endelea).


Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeshindwa kutoa majibu hayo kuhusu ahadi ya serikali ya kusambaza madawati kama ilivyoahidi.

Lissu alisema kuwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambako pia kulikuwa na ahadi ya aina hiyo, hakuna hata dawati moja ambalo lililopelekwa na hajui mpango huo uliishiwa wapi.

Awali serikali iliahidi kupeleka madawati kwa baadhi ya halmashauri za wilaya ambayo yangepelekwa kila wilaya madawati 708 ambayo madawati hayo yalikuwa katika muundo wa plastiki.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Tamisemi, George Simbachawene amesema kuwa mpango huo bado upo na kwamba, kuna shule ambazo zilipelekewa madawati kama ilivyotakiwa.

Hata hivyo amesema kuwa atapitia kuangalia ahadi katika baadhi ya maeneo ikiwemo kupeleka bungeni mkakati maalumu wa Serikali ya Awamu ya Tano utakaohakikisha kuwa tatizo la madawati kwa Shule za Msingi na Sekondari linakwisha.

Katika hatua nyingine, serikali imetoa nafasi kwa baadhi ya wazazi na wadau wengine kuchangia michango katika upatikanaji wa madawati kwa kadri watakavyoona inafaa ilimradi wasisumbue au kufanya michango hiyo iwe kizuizi cha kupeleka watoto kuendelea na masomo.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayasnsi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya wakati akijibu swali la Mbunge wa Ndanda, Cesil Mwambe (CUF).

Mbunge huyo alitaka kujua serikali imejipanga vipi kuhakikisha wanafunzi hawarudishwi shule kwa sababu ya michango ya mlinzi, madawati na chaki.

Naibu waziri amesema kuwa hakuna mkuu wa shule yeyote ambaye atamrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kutolipa michango ya mlinzi, madawati na chaki kwa sababu ya majukumu hayo ni ya Serikali.

Post a Comment

 
Top