0



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 11 Januari, 2016 amemtembelea na kumpa pole Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Frederick Sumaye ambaye amelazwa katika Taasisi ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.


Mheshimiwa Frederick Sumaye alilazwa katika Taasisi hiyo siku nne zilizopita kwa matibabu ya moyo na madaktari wanaomtibu wamemhakikishia Rais Magufuli kuwa anaendelea vizuri ikilinganishwa na wakati alipofikishwa katika Taasisi hiyo.

Pamoja na kumpa pole, Rais Magufuli pia amemuombea apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akizungumza mara baada ya kuonana na Rais, Waziri Mkuu Mstaafu Sumaye amemshukuru Rais Magufuli kwa kwenda kumuona na kueleza kuwa kitendo hicho kimeonesha jinsi alivyo na upendo wa dhati na anavyowajali watu wake.

Kuhusu hali yake, Mheshimiwa Sumaye amesema anaendelea vizuri, anapata matibabu mazuri na kwamba kwa kuwa hali yake ni nzuri anatarajia kuruhusiwa kuondoka hospitali hapo baada ya muda mfupi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
11 Januari, 2016

Post a Comment

 
Top