Wachungaji wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi
ya Victoria Nyanza (DVN) wametangaza kumfukuza kazi Askofu wa Dayosisi hiyo,
Boniface Kwangu kwa madai ya kuhusika na ubadhilifu wa Sh500 milioni.
Hii si mara
ya kwanza k
wa wachungaji wa kanisa hilo kumkataa Askofu Kwangu, baada ya mpango
kama huo kushindikana Septemba 2012 walipomtaka ajiuzulu kwa sababu mbalimbali.
Akisoma tamko
la kumfukuza kazi askofu huyo jana mbele ya waumini wa kanisa hilo, Mwenyekiti
wa wahudumu wa kanisa, Mchungaji Andrew Kashilimu alidai askofu huyo amekikuka
viapo vyake, Katiba ya Jimbo hilo, Katiba ya DVN, utumiaji mbaya wa madaraka,
mali na fedha za kanisa, kanuni na maadili ya kanisa hilo.
Mchungaji
Kashilimu alidai baada ya kikao cha wachungaji kilichofanyika Septemba mwaka
jana kilithibitisha kwamba askofu huyo hafuati kanuni na taratibu za kanisa
Anglikana Tanzania na amekuwa akiendeleza matabaka ndani ya wahudumu na waumini
na utoaji ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.
“Baada ya
kuchanganua mambo yote kwa ujumla, kikao kikaridhia Askofu Boniface Kwangu
ajiuzulu kwa ajili ya afya ya Kanisa la Mungu. Taarifa zilifika Jimbo Kuu
Anglikana Tanzania na Jimbo kupendekeza iundwe Tume ya kushughulikia mgogoro wa
DVN,” alisema Mchungaji Kashilimu na kuongeza:
“Baada ya kuundwa
kwa tume hiyo, taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya shule ya Isamilo
ambayo inamilikiwa na kanisa ilibainisha kwamba kulikuwa na upotevu wa zaidi ya
Sh500 milioni. Katika hili Askofu Kwangu alihusika na ufisadi huo.”
Kashilimu
alidai askofu huyo aligundulika kufungua akaunti binafsi katika benki ya
Mkombozi anayotumia kujipatia fedha kutoka kwa wahisani kwa kutumia jina la
dayosisi hiyo.
“Mbali na
yote alichukua dola 3,000 ambazo ni sawa na Sh6,000,000 kutoka kwa mhasibu wa
shule ya Isamilo kwa ahadi ya kuzirejesha, baada ya kudaiwa aliamua kumfukuza
kazi na mpaka sasa hajazirejesha. Kipindi cha mwaka 2008/2012 alichukua tena
Sh15,364,560 kutoka kwa mhasibu huyo nazo hajazirejesha,” alidai.
Kashilimu
alidai kutokana na tuhuma hizo Askofu huyo amesababishia dayosisi hiyo kudaiwa
na waajiriwa waliofukuzwa na kusimamishwa kazi kinyume na utaratibu wa utumishi
wa umma, hivyo kanisa hilo lina deni la zaidi ya Sh60 milioni na kwamba
ameuza gari la dayosisi hiyo.
“Kutokana na
mambo yote aliyoyafanya Askofu, kanisa limekosa imani naye na limeridhia kwa
kauli moja afukuzwe kazi, kwani amefanya ubadhirifu mkubwa kwa kanisa na kwamba
kwa kipindi cha miaka saba aliyokuwa askofu hakuna taarifa ya mapato na
matumizi aliyoitoa.
Katika hatua
nyingine Kashilimu alisema wametoa taarifa dhidi ya askofu huyo katika
Kituo cha Polisi Mkoa wa Mwanza na kupewa RB namba MW/RB/265/2016.
Hata hivyo,
Kamanda wa Polisi Mwanza, Justus Kamugisha alipoulizwa alisema hajapata taarifa
hizo na kuahidi kufuatilia tuhuma hizo kwa kuwa zinahitaji uchunguzi ili
kutolea ufafanuzi.
Juhudi za
kumpata askofu aliyeelezwa kuwa yuko nchini Marekani kwa miezi mitano sasa ili
azungumzie tuhuma hizo zilishindikana na hata alipoandikwa ujumbe kwa baruapepe
gazeti halikupata majibu hadi linakwenda mitamboni.
Pia juhudi
cha kuwapata Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jacob
Chimeledya na Katibu mkuu wa kanisa hilo, Johnson Ching’ole hazikuzaa matunda
baada ya simu zao za kiganjani kutopatikana.
Post a Comment